Mkutano mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Ijumaa Desemba 16, 2022 umemuondoa madarakani Makamu wa Rais wa chama hicho Dinah Mathaman.
Uamuzi wa kumuondoa Mathaman aliyekuwa pia kaimu rais, umefikiwa kwa sauti ya pamoja kutoka kwa wajumbe baada ya kuhojiwa na Kamu Mwenyekiti wa mkutano huo Seleman Ikomba.
Awali Mwenyekiti aliagiza Makamu wa Rais afike mbele ya mkutano kusema neno kuhusu mpishano wake na wajumbe uliotokea asubuhi hata kupelekea atimuliwe kwenye kiti chake.
"Kama Katiba inavyotutaka kumuita mtu mbele ya mkutano ili kumsikiliza, nimetuma watu wamemtafuta hayupo hapa ukumbini na simu zake zote zimezima nami napiga simpati, sasa nitamhoji," amesema Ikomba.
Baada ya kauli hiyo, amewahoji wajumbe "Wanaosema aondolewe kwenye nafasi yake waseme ndiyooo," na wajumbe waliitikia kwa sauti ya pamoja, “Ndiyooo.”
Alipowahoji wajumbe kuhusu wanaosema abaki sauti zilikuwa chache ndipo akasema waliosema ndiyo wameshinda hivyo akatangaza kuanzia leo Dinah Mathaman siyo Makamu wa Rais Tena wa CWT.
Kwa maamuzi hayo, CWT iliyokuwa chini ya Kaimu wote sasa itakuwa na viongozi wakuu bila Makamu wao.
Post a Comment