NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
JUMLA ya wanafunzi 166,438 wamepangiwa mikopo kiasi cha shilingi 424.5 bilioni na kati yao wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 68,460 na wanafunzi 97,978 ni wale wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2022/2023
Ameyasema hayo leo Desemba 14,2022 Jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda wakati wa Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Nchini Tanzania yaliyofanyika katika Chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu hadi kufikia shilingi 654 bilioni kutoka shilingi 570 bilioni za awali, sawa na ongezeko la asilimia 14.7 ambazo zinaenda kusaidia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi ambao wapo vyuoni.
Aidha wamekuwa wakitenga bajeti kwa ajili ya motisha kwa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wanaochapisha tafiti zao katika majarida makubwa duniani ili waweze kutambulika ulimwenguni kama watafiti wabobezi.
“Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imetenga shilingi Bilioni moja, ambapo kila mtafiti atakayekidhi vigezo atapata shilingi milioni 50”. Amesema Prof.Mkenda.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Nchini Tanzania, Prof.Eliab Opiyo amesema Chuo kimejipanga kuanzisha masomo ya Shahada ya uzamili na uzamivu katika mwaka wa masomo 2022/2023 kwa kukamilisha uandishi wa mitaala inayokidhi mahitaji ya sasa na ya siku za mbeleni.
Hata hivyo amewataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwatumikia Watanzania kwa nidhamu na uadilifu “Chukieni rushwa, zingatieni na kutii sheria, na tendeni haki”.
Amesema Chuo kimefanya juhudi mbalimbali kuzidi kuongeza ubora wa elimu inayotolewa chuoni ikiwemo kuendesha Chuo kufuatana na Mpango Mkakati wa Chuo wa miaka 5 (2021/22-2025/26) ambao unasisitiza kuandaa wahitimu mahiri na wenye ubunifu ili kuchangia katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa juu zaidi.
Post a Comment