" PAROKIA YA NGOKOLO YATOA MSAADA KWA WALEZI YA SHIRIKA LA KITAWA LA JIMBO KATOLIKI SHINYANGA

PAROKIA YA NGOKOLO YATOA MSAADA KWA WALEZI YA SHIRIKA LA KITAWA LA JIMBO KATOLIKI SHINYANGA

 

Uongozi wa Parokia ya Ngokolo katika Jimbo Katoliki Shinyanga, umekabidhi msaada wa vitu mbalimbali katika nyumba ya malezi ya shirika la Watawa la Kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma, iliyopo mtaa wa Miti mirefu (Uzunguni) katika Manispaa ya Shinyanga.

Vitu vilivyokabidhiwa ni pamoja na kilo 300 za mchele, lita 60 za mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia zenye thamani ya Shilingi Laki 1 na 78 Elfu, Kilo 100 za Sukari, taulo za kike na Fedha taslimu kiasi cha Shilingi laki mbili na hamsini Elfu.

Akikabidhi vitu hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni moja na laki nane, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia ya Ngokolo Luteni Kanali Mstaafu John Kayoka, amesema msaada huo ni kwa ajili ya kuwasaidia mabinti walioko katika malezi ya kitawa kusherehekea sikukuu ya Krismasi, ikiwa ni sehemu ya majitoleo ya Parokia ya Ngokolo kwa wahitaji .

Kayoka ametumia nafasi hiyo kuziomba Parokia zingine kujitokeza kuitegemeza nyumba hiyo ya malezi, ikiwa ni hatua ya kumsaidia Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kuwalea mabinti ambao wako katika hatua ya malezi ya kitawa.

Naye Katibu wa Halmashauri walei Parokia ya Ngokolo Bi.Elda Nkulu, amesema wametoa msaada huo kwa kuwa Walelewa hao ni sehemu ya watu wenye uhitaji wa kusaidiwa vitu mbalimbali.

Kwa upande wake mlezi mkuu wa mabinti hao Sister Regina Lusimo, amewashukuru Waamini wa Parokia ya Ngokolo kwa kuwakumbuka na kutambua mahitaji waliyonayo, huku Walelewa hao wakiushukuru uongozi wa Parokia ya Ngokolo kwa moyo wao wa upendo, kwa kuona umuhimu wa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) jimbo za kuwategemeza.

Shirika la kitawa la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma, lilianzishwa miaka michache iliyopita na Askofu wa Jimbo katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kwa Ajili ya kuwaandaa mabinti wenye nia thabiti ya kumtumikia Mwenyezi Mungu kuwa Watawa wa Jimbo, ambao kupitia maisha ya wakfu watajitoa sadaka na kufanya kazi mbalimbali za utume wa Kanisa, katika Jimbo la Shinyanga na maeneo mengine.

Shirika hilo kwa sasa limekabidhiwa kwa WAWATA jimbo, ambapo pamoja na mambo mengine wamepewa jukumu la kuongoza shughuli za kulitegemeza kwa kushirikiana na watu wengine wenye mapenzi mema.

Tangu wakabidhiwe jukumu hilo, WAWATA jimbo la Shinyanga wamekuwa wakijitoa kwa moyo wa pekee na wa upendo katika kulitegemeza shirika hilo, kwa kushirikiana na Watu mbalimbali wenye mapenzi mema ikiwemo kama wana Parolia ya Ngokolo.

Walelewa wakipokea vitu mbalimbali kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia ya Ngokolo Luteni Kanali Mstaafu John Kayoka (Mwenye kaunda suti)na kutoa shukrani zao
Mlezi Msaidizi Sister Elizabeth Ndahwera akipokea msaada wa fedha taslimu kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia ya Ngokolo Luteni Kanali Mstaafu John Kayoka
Walelewa wa Shirika la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma wakifurahia mara baada ya kukabidhiwa zawadi mbalimbali na uongozi wa Parokia ya Ngokolo
Mlezi mkuu Sister Regina Lusimo akitoa neno la Shukrani kwa Uongozi na Waamini wa Parokia ya Ngokolo kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia ya Ngokolo Luteni Kanali Mstaafu John Kayoka na Katikati ni Katibu wa Parokia Bi.Elda Nkulu
Walelewa wakiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Halmashauri Walei Parokia ya Ngokolo mara baada ya kukabidhiwa msada kwa ajili ya sikukuu

Post a Comment

Previous Post Next Post