" SHIRIKA LA KTO, CHUO CHA FDC NA TAKUKURU WAIMARISHA WANANCHI SHINYANGA JUU YA RUSHWA YA NGONO SHINYANGA

SHIRIKA LA KTO, CHUO CHA FDC NA TAKUKURU WAIMARISHA WANANCHI SHINYANGA JUU YA RUSHWA YA NGONO SHINYANGA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization  (KTO) kwa kushirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Buhangija limewajengea uwezo wa kupambana na  Rushwa ya ngono Chama cha waendesha baiskeli na waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga.

Mafunzo hayo yametolewa Ijumaa Desemba 16,2022  katika ukumbi wa Mama Samia  Shule ya Msingi Buhangija  Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization KTO Maggid Mjengwa amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na waendesha baiskeli hivyo amewataka kuwa mabalozi katika kuelimisha jamii ili kutokomeza  rushwa ya ngono.

“Ninyi mliopo hapa na zaidi wanahabari mkipata uelewa wa juu ya jambo hili mtaweza kuisaidia jamii nanyi waendesha baiskeli mnatakiwa muwe mabalozi wazuri wa kufikisha elimu ya kupambana na rushwa ya ngono katika jamii”,amesema Mjengwa.

 

Kwa upande wake Afisa Uchunguzi TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Reubeni Chongolo amesema mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ikiwemo ya rushwa ya ngono yanaweza kukomeshwa endapo jamii itasimama na kuzingatia  maadili mema.

“Sababu pekee ya kuendelea kuwepo kwa rushwa ni mmomonyoko wa maadili kwahiyo watumishi na watu wote ambao wako kwenye nafasi za kuweza kutoa huduma wanapokosa kuwa na maadili hupelekea kuomba au kupokea rushwa jambo la msingi ambalo tunahimiza lazima tusimame kwenye misingi ya uadilifu”.amesema Chongolo

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja amesisitiza jamii kutofumbia macho vitendo vya rushwa na kwamba jamii  inapaswa kutoa taarifa sahihi ili TAKUKURU iweze kuchukua hatua.

Hata hivyo Mkuu wa Chuo cha FDC Buhangija Maria Mkanwa amesema elimu iliyotolewa ni msaada mkubwa katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.   

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamepata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa papo kwa hapo na wataalam kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya rushwa ya ngono.

Baadhi ya washiriki hao wamelipongeza shirika la KTO kwa kutoa elimu hiyo ya rushwa ya ngono ili iwasaidie katika maisha yao ya kila siku pamoja na kusaidia jamii.

Mafunzo ya elimu ya rushwa ya ngono yametolewa siku ya Ijumaa  Disemba 16,2022 na kwamba yameratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization KTO.










Post a Comment

Previous Post Next Post