Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Rai imetolewa kwa wananchi wote wa mtaa wa Dome Kata ya
Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kuendelea
kushirikiana na uongozi wa serikali ya mtaa huo ili kuwabaini wahalifu kwa
lengo la kuimarisha usalama.
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa mtaa wa Dome Bwana Solomon Najulwa kwenye Mkutano wake wa hadhara wa robo mwaka ambao
umelenga kutoa taarifa za mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kupokea kero
mbalimnbali za wananchi.
Bwana Najulwa amesema wananchi
wanapaswa kuendelea kutoa taarifa
pindi wanapobaini viashiria vya uhalifu na wahalifu ili uongozi huo uweze
kushughulikia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ambalo lipo kwaajili ya
kulinda usalama wa raia na mali zao.
Wakati huo huo Bwana
Najulwa amewasisitiza wakazi wa mtaa huo kuzingatia kanuni na taratibu za
kuwatambulisha wageni wanaofika kwenye familiza zao katika uongozi wa serikali
ili waweze kufahamika jambo ambalo litasaidia kuimarisha ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine baadhi
ya wakazi wa mtaa wa Dome wamewaomba wananchi wengine kuwafikisha sehemu husika
wageni wanaofika kwenye familia zao ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.
Katika taarifa yake ameelezea mambo mbalimbali
yaliyofanywa na uongozi wa serikali ya mtaa kwa kipindi cha miezi mitatu
kuanzia Januari hadi mwezi huu Machi mwaka 2023.
Amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kutambulisha
wananchi 115 kupata mkopo katika taasisi za kifedha, waliotambulishwa katika
maombi mbalimbali ya kazi 316 na uongozi huo kutatua changamoto 57 za wananchi
zinazohusu dawati la Polisi.
Mwenyekiti Najulwa amesema wamewezesha wananchi
takribani 275 kupata utambulisho wa Uraia wa NIDA huku akieleza kuwa kwa
kipindi hicho uongozi huo umesimamia huduma vizuri kwa walengwa wa TASAF na
kusuluhisha migogoro midogomidogo takribani 340 na kusaidia wananchi hao
kuendelea kuishi kwa amani.
Amesema kwa upande wa miundombinu ya barabara ujenzi
unaendelea vizuri ambapo ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine mtaa huo umeendelea
kusimamia uwekaji wa vibao vya barabarani kwa ajili ya kutambulisha eneo husika.
Bwana Nalinga jina maarufu Cheupe amesema uongozi huo pia umeshirikiana
vizuri na wazazi kuhusu elimu ya watoto kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu juu
ya maadili mema kwa watoto huku akieleza kuwa hakuna changamoto ya usafi wa
mazingira na kwamba katika suala la afya uongozi huo umewaandikia barua za
msamaha wa matibabu ya bure wazee 35 wenye miaka kuanzia 60.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Dome wamewaomba wananchi wengine kuwafikisha sehemu husika wagani wanaofika kwenye familia ili kuepukana na changamoto.
Post a Comment