Na Elisha Petro, Misalaba
Blog
Kamanda wa jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amelitaka
jeshi la jadi Sungusungu kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa
kuzingatia sheria na taratibu za Nchi.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na
jeshi la jadi sungusungu wa kata ya Ndala kwenye semina elekezi juu ya
utendaji kazi, ambayo imeandaliwa na Diwani wa kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani ambapo pamoja na mambo mengine amewakumbusha Sungusungu kutojichukulia sheria
mkononi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kamanda Magomi amesema
serikali inatambua juhudi za sungusungu katika kukabiliana na uhalifu na
wahalifu lakini amesisitiza kuzingatiwa kwa uzalendo na weledi pamoja na kuendelea
kushirikiana na jeshi la polisi ktk
jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi.
“Kiukweli
mnafanyakazi nzuri katika kukahikisha
maeneo yetu, mali na watu wetu wote wanakuwa salama hii ni faida ambayo sisi
jeshi la Polisi tunaitambua na kuithamini
sana niendelee kuwataka
mfanyekazi hii huku mkitanguliza uzalendo”.
“Niwaase
wapiganaji na makamanda wangu wa sungusungu tufanyekazi yetu kwa weledi wa hali
ya juu na kwa kuzingatia sheria za Nchi na nawaahidi ushirikiano wa dhati
lakini pia ofisi zetu ziko wazi muda wote pale ambapo unatendewa ndiyo sivyo
sema sisi tutachukua hatua”.amesema kamanda Magomi.
Aidha kamanda Magomi
ametumia nafasi hiyo kuiomba jamii hasa wazazi na walezi kuendelea kushirikiana
na serikali katika kutokomeza mmomonyoko wa maadili na kuimarisha ulinzi na
usalama.
Kwa upande wake Diwani wa
kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani amewasihi
jeshi la sungusungu kata hiyo kuendelea kushirikiana katika juhudi za kuimarisha
usalama kwa wananchi.
“Tuendelee
kudumisha upendo, tuendelee kushirikiana kwa pamoja, tuendelee kusheshimiana
kwa nafasi zetu ili safari yetu iwe njema pamoja na kwamba tunahamasisha
masuala ya maendeleo hatuwezi kupata maendeleo bila kuwa na usalama lakini
niseme makamanda hawa wanatusaidia sana kata ya Ndala niombe tu tuendelee
kushirikiana huku tukimtanguliza mwenyezi Mungu”.amesema
Mhe. Zamda
Akisoma risala
iliyoandaliwa na jeshi la Sungusungu kata ya Ndala katibu wa jeshi hilo Bwana
Raymond Misana ameelezea mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na kuahidi kuendelea
kushirikiana na jeshi la polisi katika utekelezaji wa majukumu.
“Sungusungu
kata ya Ndala pamoja na matukio madogomadogo kwenye mitaa yetu tumefanikiwa
kuzuia matukio makubwa yaliyokuwa yakijirudia kama vile wizi wa mifugo, kuvunja
na kuiba, upolaji wa simu za mikononi na mikoba ya akina mama kwa kutumia
bodaboda na matukio mengine’
“Kwa
kiasi kikubwa uhalifu mdogomdogo unaotokea kwa sasa unachangiwa na uzembe wa
watu wanaotendewa uhalifu huo ama kwa kutoweka taa za ulinzi kwenye nyumba zao
au kwa kutofunga milango na mageti nyakati za usiku pia tunaahidi kuendelea
kupokea na kufanyika kazi maelekezo yako kutoka jeshi la Polisi”
Semina hiyo imefanyika
katika soko la Ndala na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa kata pamoja na jeshi la polisi ambapo mgeni rasmi alikuwa kamanda wa jeshi
la polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi.
Kamanda wa jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akisoma hotuba kwenye
semina iliyoandaliwa na Diwani wa kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani.
Diwani wa kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani akiomba ushirikiano kwa
jeshi la sungusungu kata hiyo.
Diwani wa kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani akizungumza kwenye semina
hiyo
Katibu wa jeshi hilo
Bwana Raymond akisoma risala iliyoandaliwa na jeshi la Sungusungu kata ya Ndala.
Semina elekezi juu ya
utendaji kazi, ambayo imeandaliwa na Diwani wa kata ya Ndala Mhe. Zamda Shabani ikiendelea katika soko la Ndala Manispaa ya Shinyanga.
Post a Comment