" KAMATI TENDAJI YA CHADEMA YAMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA CHAMA SHINYANGA, MHE. MTOBI AKANUSHA HAJAPOKEA BARUA RASMI

KAMATI TENDAJI YA CHADEMA YAMSIMAMISHA UONGOZI MWENYEKITI WA CHAMA SHINYANGA, MHE. MTOBI AKANUSHA HAJAPOKEA BARUA RASMI


Kamati tendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kanda ya Serengeti kimemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi kutokana na tuhuma za makosa ya kinidhamu.

Akizungumza Katibu wa kamati ya uenezi wa CHADEMA Kanda ya Serengeti Golden Marcus amebainisha kuwa kamati tendaji ya Chama hicho imemsimamisha Mheshimiwa Ntobi kutojihusisha na shughuli zozote za uongozi kwa kipindi cha Mwaka mmoja.

Aidha Kamati hiyo imemvua uongozi aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Ndugu Emmanuel Buyamba ambaye pia anatuhumiwa kwa makossa ya kinidhamu.

“Kikao kilifanyika Tarehe 28, 4,2023 pamoja na Tarehe 29,4,2023  pamoja na mambo mengine ya kichama yaliyojadiliwa kwenye vikao hivyo, kamati tendaji iliamua kumsimamia uongozi Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi na vilevile kutojihusisha na shughuli zozote za kiuongozi kwa muda wa miezi kumi na mbili (12) hii yote ni kutokana na makosa ya kinidhamu ndani ya chama”.

“Lakini pia kamanti tendaji ilimvua uongozi aliyekuwa katibu wa Mkoa wa Shinyanga Ndugu Emmanuel Buyamba naye pia ni kutokana na makosa ya kinidhamu barua tayari walishapokea”.amesema katibu wa kanda Marcus

Pamoja na hatua hiyo Bwana Marcus amebainisha kuwa viongozi hao bado wanaendelea kutambuliwa kama wanachama halali wa CHADEMA na wana haki ya kukata Rufaa kwa ngazi za juu kupinga hatua zilizochukuliwa.

Misalaba Blog imezungumza pia na Mwenyekiti wa CHADEMA aliyesimamishwa uongozi Bwana Emmanuel Ntobi ambaye amesema hajapata barua rasmi wala nakala ya hukumu ya adhabu iliyotolewa na chama chake.

“Mpaka sasa hivi tunavyoongea sijapata barua yoyote ya kusimamishwa wala sijapata nakala ya hukumu ya hiyo adhabu iliyotolewa bahati mbaya nasikitika sana katibu wa kamati ya uenezi ameongea kwamba amekwisha nipatia hiyo barua na nakala ya hukumu huu ni mwendelezo tu wa kuona uongozi wa kanda kunashida kubwa tangu taarifa hiyo itoke siku nne zimepita mimi sijapata barua rasmi wala nakala ya hukumu bado nasubiria nikishapata barua rasmi na nakala ya hukumu nitajua na mimi hatua gani nachukua kwahiyo wakileta hivo vitu nitafanya maamuzi na mimi”.amesema Mhe. Ntobi

Hata hivyo hazikufanikiwa juhudi za kumpata aliyekuwa katibu wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga Bwana Emmanuel Buyamba ambaye licha ya kupigiwa simu lakini iliita bila kupokelewa.

Post a Comment

Previous Post Next Post