" WANANCHI KOLANDOTO KUPATA HATIMILIKI NA FIDIA ZAO, MHE. MEYA MASUMBUKO AAGIZA WATENDAJI WA KATA MANISPAA YA SHINYANGA

WANANCHI KOLANDOTO KUPATA HATIMILIKI NA FIDIA ZAO, MHE. MEYA MASUMBUKO AAGIZA WATENDAJI WA KATA MANISPAA YA SHINYANGA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imesema kwa  Mwaka wa fedha 2023/2024  itaanza kupima maeneo ya wananchi ambao tayari wameshalipia kwa ajili ya kupata hatimiliki zao pamoja na wananchi wanaodai fidia kwenye utanuzi wa eneo la chuo cha afya Kolandoto.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bwana John Tesha kwenye  kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo  wakati akijibu swali la diwani wa kata ya Kolandoto Mhe. Mussa Elias aliyetaka kujua ni lini wananchi wa kata hiyo watapimiwa maeneo yao ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia kwa wananchi watakaopisha utanuzi wa Chuo cha afya Kolandoto.

“Wananchi wa kata ya Kolandoto wameshalipa fedha kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao fedha hizi zimelipwa imepita Miaka mitano sasa na hili swali nimekuwa nikiliuliza mara kwa mara kwenye baraza na sasa kwa kuwa tunaingia kwenye Mwaka mwingine tena naomba nipate majibu wananchi wa Kolandoto ni lini watakwenda kupimiwa ardhi zao na kupata hati zao kwa ajili ya manufaa ya familia zao”.

“Kolandoto tunahitaji kupanua chuo kuwa chuo kikuu wananchi wa maeneo yale wamekwishakutwaliwa maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho swali langu kwa sababu mchakato huu ulisimamiwa na Manispaa je ni lini sasa hao wananchi wanakwenda kulipwa fidia zao kwa sababu ni muda mrefu sasa umepita toka waahidiwe fidia zao hizi”.Amesema Mhe. Diwani Elias

Kaimu Mkurugenzi Bwana Tesha amesema Halmashauri hiyo imepanga kuanza kupima maeneo ya wananchi ili kuwapatia hatimiliki zao huku akibainisha zoezi la kulipa fidia wananchi watakaopisha kwa ajili ya utanuzi wa eneo la chuo hicho.

“Ni kweli wananchi wa Kolandoto walihamasishwa kufanya uchangiaji kwa ajili ya kufanyiwa upimaji au urasimishaji wa maeneo yao sasa eneo lote la Kolandoto limeingizwa kwenye mradi unaoitwa uboreshaji miliki salama Nchini na mradi huu unafadhiriwa na Benki ya Dunia na utaanza rasmi Tarehe moja (1) kwezi wa saba (7) Mwaka huu 2023”

“Mheshimiwa Diwani ameuliza juu ya wananchi wanaozunguka chuo kile cha afya Kolandoto ambapo eneo la wananchi wale limeshapimwa lakini wananchi wale hawajalipwa fidia ni kweli zoezi hilo limeshafanyika na tayari taarifa za wananchi hao zimeshachukuliwa taarifa hizo zimeingizwa kwenye vikao rasmi vya kamati ya mipango miji takwimu ziko tayari na Mwaka wa fedha ujao wananchi wale wataanza kulipwa”.amesema Bwana Tesha

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Bwana Elias Masumbuko pamoja na mambo mengine amekemea na kuagiza watendaji wa kata kwenda kwenye shule mbalimbali ili kubaini michango inayochangishwa bila kufuata utaratibu.

“Kuna maeneo mawili yanasema ukaguzi wa shule ni kama kata tatu au mbili zinaonyesha kama kuna shule zimekaguliwa kumbe katika kila robo hatuoni utendaji wa kazi katika sekta hii kuna malalamiko mengi wazazi wanalalamika kwenye kata watoto wanaambiwa kununua rimu kwenye kata huko watendaji mtusaidie kuna michango mia tano mia tano mwalimu anaagiza za mitihani kwa nini hizo mia tano mia tano za nini mwalimu anasema ni kwa ajili ya kuandalia mtihani watendaji wa kata mtusaidie  mtihani upi huo kama kuna maelekezo hayo TAMISEMI mtuambie sasa na hawa wanaokagua kwenye shule wanakagua majengo au wanakagua nini watendaji wa kata ndiyo wasaidizi wa mkurugenzi fuatilieni hili jambo kuna malalamiko mengi sana kwa wazazi”.amesema Meya Masumbuko

Mstahiki Meya huyo Mhe. Masumbuko amewasihi madiwani wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kushirikiana na wazazi katika suala la kusimamia maadili mema ili kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Amewashauri wazazi na walezi wa watoto katika shule mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga kwenye vikao vyao kuweka sheria na kanuni ndogondogo zitakazowaelekeza wazazi kuwajibika na lishe ya watoto shuleni.

Leo Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limekaa kikao cha robo ya tatu kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha madiwani wa kata zote za Manispaa ya Shinyanga wamewasilisha taarifa ikiwemo changamoto zilizopo kwenye kata zao huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini naibu waziri ofisi ya waziri Mkuu kazi,vijana,ajira na wenye ulemavu Mhe. Paschal Patrobas Katambi kwa kuendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto za wananchi.Mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko akizungumza kwenye baraza hilo leo Mei 3,2023.Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bwana John Tesha akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye baraza hilo la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo Mei 3,2023.Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe akizungumza kwenye baraza la matiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo Mei 3,2023.Diwani wa kata ya Kolandoto Mhe. Mussa Elias akiuliza swali leo kwenye baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.Diwani wa kata ya Kambarage mjini Shinyanga Mhe. Hassan Mwendapole akizungumza leo kwenye baraza la madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.Diwani wa kata ya Mwamalili Mhe. James Matinde Mdimi akizungumza leo kwenye baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.




Post a Comment

Previous Post Next Post