Na Mapuli Kitina Misalaba
Hatua ya robo
fainali ya Ligi ya Makamba Lameck maarufu kama Krismas Cup 2024 imetamatika leo Desemba 11, 2024 katika uwanja wa Mhangu, kata ya Salawe, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, huku
Salawe FC ikiibuka kidedea dhidi ya Mwabenda FC kwa ushindi wa magoli 2-0.
Magoli ya ushindi wa Salawe FC yamefungwa na Paschal
Neymer Jr dakika ya 43 na 68, na kuipa timu hiyo tiketi ya kucheza nusu fainali
inayotarajiwa kufanyika Jumatatu, Desemba 16, 2024.
Akizungumza kwa niaba ya msimamizi wa ligi hiyo,
Bwana Paul Daud, maarufu kama MC Niache Kona, amesema mechi ya kesho ni nusu fainali
ya kwanza kati ya Beya FC na Kano FC, huku akitoa wito kwa wananchi kumuunga
mkono mwandaaji wa ligi hiyo, Bwana Makamba Mussa Lameck.
"Ligi
hii imeleta mvuto mkubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla. Michezo ni ajira na
pia ni afya. Niwaombe wananchi na wapenzi wa michezo tujitokeze kwa wingi
kushuhudia mechi hizi na kumsapoti kijana Makamba Lameck ambaye ameanzisha ligi
hii kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana,"
amesema MC Niache Kona.
Kwa upande wake, mgeni rasmi wa mechi ya leo, mdau
wa michezo Bwana Raphael Sayi Felisian, amepongeza maandalizi ya ligi hiyo na
kuwasihi vijana wanaoshiriki kuendelea na juhudi zao.
"Ligi
hii inaleta burudani na ushindani mzuri. Nampongeza Bwana Makamba Mussa Lameck
kwa juhudi zake. Vijana kupitia ligi hii wanaweza kufikia ngazi za juu zaidi na
kupata ajira. Ni jambo la kujivunia kuona michezo inaendelea kwa amani na
utulivu," amesema Raphael.
Aidha, wazee wa kijiji cha Songambele, wakazi wa
Mhangu kata ya Salawe wamesema kuwa ligi hiyo ni hatua kubwa ya kuwasaidia
vijana kuepuka makundi mabaya kama utumiaji wa dawa za kulevya huku wakimpongeza
Makamba Mussa Lameck na kumhimiza aendelee kuandaa mashindano kama hayo kwa
ubunifu zaidi.
Mashindano haya yanadhaminiwa na Makamba Mussa
Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka ambapo
ligi hiyo inalenga kukuza vipaji vya michezo na kuchochea maendeleo ya
kimichezo mkoani Shinyanga.
Fainali za Krismas Cup zinatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba 2024, ambapo zawadi zitatolewa kwa washindi wa nafasi ya kwanza hadi ya tatu.
Post a Comment