Na Neema Kandoro MISUNGWI
ZAIDI ya wakulima 800 wamenufaika bure na elimu ya kilimo bora inayotolewa na Chuo Cha Mafunzo ya Kilimo Ukiruguru kilichopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza kwa ushirikiano na Taasisi zingine za kilimo.
Hayo yamebainishwa kwenye Chuo Cha Ukiruguru na Kaimu Mkuu wa chuo hicho Kiva Francis Mbemba akisema kuwa mafunzo hayo yameanza mwezi wa saba mwaka jana baada ya Mhe, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
kukitaka chuo hicho kutoa mafunzo bure kwa wakulima.
Alisema wakulima kutoka maeneo tofauti wanaojishughulisha na Kilimo cha mpunga, pamba, alizeti, viazi vitamu, karanga, mahindi, choroko na mbogamboga wanafika katika chuo hicho kupata mafunzo.
Kiva alisema kuwa Shirika la kimataifa la Ushirikiano Japan (JICA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Shirika la Afya ya Mimea na Mamlaka ya Viuatilifu (TPHPA) wamekuwa wakiwaleta wakulima kutoka maeneo tofauti kuungana na wale walio karibu kwenye chuo hicho kupata mafunzo ya kilimo.
"Wakulima wanaopata mafunzo hapa ni kutokea hapa kwetu Mwanza, Geita, Shinyanga na Mara ambao huletwa na hayo mashirika sisi chuo tunatumia matangazo ili wakulima wengine wafahamu fursa hiyo hivyo hujumuika na wenzao"alisema Kiva
Alisema hatua hiyo inawezesha kuwajengea wakulima misingi mhimu ya elimu ya kilimo ambayo itawafanya kuweza kupata tija kwenye shughuli yao hiyo waifanyayo na kuweza kuwa na usalama wa chakula.
Kiva alisema kilimo ni biashara na ajira hivyo wakulima pamoja na maafisa ugani wanayo fursa kubwa ya kuja kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna gani bora ya kufikia kupata mafanikio makubwa kwenye sekta hiyo.
Aidha Kaimu huyo wa chuo amewataka wakulima kuwa na utashi wa kupata mafunzo ya kilimo bora kwani itawawezesha kuongeza mavuno yao shambani na hivyo kupata maendeleo yao binafsi na taifa.
Post a Comment