" Tundu Lissu na Wenzake Waachiwe Bila Masharti - Kanisa Katoliki

Tundu Lissu na Wenzake Waachiwe Bila Masharti - Kanisa Katoliki

 Tundu Lissu na Wenzake Waachiwe Bila Masharti - Kanisa Katoliki


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuwaachilia mara moja na bila masharti viongozi wa kisiasa waliokamatwa kwa kudai haki, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani ya taifa, hasa kuelekea mwaka wa uchaguzi.


Rais wa TEC na Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, amesema kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa kutumia nguvu bali kwa maridhiano na haki, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani ya nchi kwa kuhakikisha mifumo ya uchaguzi inarekebishwa ili kutoa nafasi kwa upatikanaji wa viongozi wa haki na wa kweli.


“Katika hali ya kawaida, nani anaharibu amani? Anayetumia nguvu na kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka yeye au yule anayesema ‘jamani turudi mezani ili tuangalie mifumo yetu ya uchaguzi kwani mifumo ya sasa haiwezi kutupatia viongozi wa haki na kweli’?” amehoji Askofu Pisa.


Akizungumza katika mkesha wa Pasaka uliofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Kagwa, Jimbo Katoliki Lindi, Askofu huyo amesema kuwa kama kurudi mezani ndiko kunakoweza kulinda amani, basi kila anayehamasisha hilo anapaswa kuungwa mkono, si kukandamizwa au kukamatwa.


“Kwa maana hiyo wote waliokamatwa kwa kudai haki, wakiwemo viongozi wa vyama vya kisiasa, waachiwe haraka na bila masharti, na wengine wasikamatwe wala kusumbuliwa. Pia mihimili isiingiliwe bali itende kazi zake kwa haki,” amesisitiza.


Amesema kuwa amani ni tunu adhimu inayopatikana kwa gharama kubwa, hivyo haipaswi kuchezewa, huku akisisitiza kuwa taifa linapaswa kuikataa dhana ya kuimba wimbo wa amani isiyotokana na haki.


Kauli ya Askofu Pisa imekuja wakati ambapo mjadala wa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na ushiriki wa vyama vya siasa umekuwa ukitawala anga ya kisiasa nchini, huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu kukamatwa kwa viongozi wao wakubwa akiwamo Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Tundu Lissu, na ukosefu wa haki katika uendeshaji wa siasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post