" MAKALA: WAKAZI WA BUSHOLA MANISPAA YA SHINYANGA WALIA NA MAJI MACHAFU: WACHANGIA NA WANYAMA, WAOMBA MAJI SAFI KUEPUKA MAGONJWA

MAKALA: WAKAZI WA BUSHOLA MANISPAA YA SHINYANGA WALIA NA MAJI MACHAFU: WACHANGIA NA WANYAMA, WAOMBA MAJI SAFI KUEPUKA MAGONJWA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Katika kijiji cha Bushola na Lyandu, kilichopo kata ya Mwamalili, Manispaa ya Shinyanga, maji yamekuwa kama lulu isiyoonekana ambapo wakazi wa vijiji hivi wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya upatikanaji wa maji safi na salama, hali inayowalazimu kutumia maji ya bwawa la asili linalotumiwa pia na mifugo kama Ng’ombe na Mbuzi, jambo ambalo linahatarisha afya zao kwa kiwango kikubwa.

MISALABA MEDIA ilifika katika eneo hilo na kushuhudia wanawake na watoto wakichota maji kutoka kwenye bwawa hilo huku likitumika na wanyama hao na kwamba wakazi hawa, maji ya bwawa siyo chaguo mbali  ni suluhisho la dharura kutokana na ukosefu wa huduma bora ya majisafi.

“Hili bwawa tunalitumia sisi binadamu na wanyama. Hakuna kisima wala bomba la maji hapa. Watoto wanaugua minyoo, kuhara na wengine ngozi zinapauka. Tumechoka,” alisema Evaline Luzwilo mkazi wa Lyandu.

Wenyeviti wa vijiji na watendaji waliozungumza na MISALABA MEDIA walithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo kwa muda mrefu, huku wakisema kuwa jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika, lakini bado hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.

Wakazi wa maeneo hayo wameomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia huduma ya maji kutoka Ziwa Viktoria, kama njia ya kudumu ya kuwahakikishia maji safi. Wanadai kwamba hakuna sababu ya wao kuendelea kutumia maji yasiyo salama ilhali ziwa hilo kubwa liko karibu na mkoa wa Shinyanga.

“Tunaomba Serikali ituangalie sisi wa vijijini. Tumevumilia vya kutosha. Kama bomba linaweza kufikishwa Shinyanga mjini na Kishapu, kwa nini lisitufikie Bushola na Lyandu?” alihoji Lazaro Masele, mkazi wa Bushola.

Kwa wakazi wa Bushola na Lyandu, maji ya bwawa si tu hitaji – ni jambo la kulazimika. Katika hali ya kushangaza na kusikitisha, familia nyingi zinabeba madumu wakati wakielekea kwenye bwawa moja tu linalopatikana maeneo ya jirani. Katika bwawa hilo inaelezwa kuwa wenda wanyama kama Fisi wanatumia hasa nyakati za usiku kwa kuwa huonekana katika maeneo hayo.

“Tunaogopa lakini tunaishi kwa mazoea. Hakuna maji ya bomba hapa. Tunasumbuliwa na magonjwa kila wakati, Watoto wanapata minyoo, kuhara, na hata magonjwa ya ngozi kwa sababu ya haya maji,” anasema Anastazia Shiku , mkazi wa Bushola.

Diwani wa kata ya Mwamalili, Mhe. James Matinde, hakusita kueleza ukweli ambapo alisema changamoto ya maji imekuwa sugu na juhudi nyingi zimekuwa zikifanyika kwa nyakati tofauti, lakini majibu rasmi ya utekelezaji wa mradi wa maji hayajawahi kutolewa kwa ukamilifu.

“Hili ni tatizo linaloendelea. Tumeshawasiliana na mamlaka husika, hasa SHUWASA, lakini mpaka sasa hatujapewa tarehe halisi ya kuanza kwa mradi wa kuwapatia wananchi maji ya uhakika. Wananchi wamechoka. Tunahitaji msaada wa haraka,” alisema Mhe. Matinde.

Baada ya malalamiko kuendelea kuongezeka, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeeleza kuwa inatambua changamoto hiyo na inafanya kila jitihada kuhakikisha maji kutoka Ziwa Viktoria yanawafikia wakazi wa Bushola na Lyandu.

Kwa mujibu wa Mhandisi Uswege Musa, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Maji SHUWASA, tayari kuna mpango wa kuunganisha bomba kubwa linalosafirisha maji kuelekea wilaya ya Kishapu ili liweze kutawanya tawi kuelekea Bushola.

“Changamoto ipo. Kisima cha maji marefu kilichopo Mwagala kina maji yenye chumvi, na wananchi hawataki kuyatumia. Ndiyo maana sasa tunalenga kutumia mfumo wa maji kutoka Ziwa Viktoria. Mpango huu ni wa muda mfupi, lakini kuna pia mradi mkubwa wa muda mrefu,” alisema Mhandisi huyo.

SHUWASA kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Serikali ya Tanzania, imeandaa mradi wa kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu mabilioni ya fedha na utahusisha:Kubadilisha mabomba chakavu yenye urefu wa kilomita 9, Kufunga mabomba mapya ya maji yenye urefu wa zaidi ya kilomita 35, Kufikia vijiji vya pembezoni kama Bushola, Lyandu, Iselamagazi, Mwagala na vingine

Kwa sasa, SHUWASA imemaliza hatua ya kupata mshauri mtaalamu wa mradi, na kinachosubiriwa ni mkandarasi ambaye ataanza utekelezaji.

“Tunaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu. Serikali yao kupitia SHUWASA ipo makini na tunahakikisha hili linashughulikiwa kwa haraka,” aliongeza Mhandisi Uswege.

Licha ya matumaini hayo mapya, bado wananchi hawana imani ya haraka. Wengi wanasema wamekuwa wakisikia ahadi kwa muda mrefu bila matokeo ya wazi. Hata hivyo SHUWASA haijataja terehe ya kuanza utatuzi wa changamoto hiyo ya maji ambapo wananchi wanaendelea kutoa  wito kwa viongozi wa serikali, mashirika ya maendeleo na mashirika ya haki za binadamu kufika kuona hali halisi.

“Hii siyo maisha ya binadamu. Tunaomba viongozi wasikae ofisini wakisoma ripoti, wafike hapa waone tunavyoteseka,” alisema Mzee Charles Dotto, mkazi wa Bushola.

Katika dunia ya sasa ambapo lengo namba sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6) linataka “Upatikanaji wa maji safi na huduma za kujisafi kwa wote ifikapo 2030,” ni aibu kuona wakazi wa maeneo ya mijini kama Shinyanga bado wakitegemea maji ya mabwawa ya wanyama.

Mwenyekiti wa kijiji cha Bushola Edward Machiya Lyokala anatoa wito kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini na mashirika ya kiraia kushirikiana kuhakikisha maji safi yanapatikana kwa wakazi wa Bushola na Lyandu haraka iwezekanavyo.

Wakati hayo yakiendelea Shinyanga, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewasilisha bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo ametaja vipaumbele saba ambavyo serikali inatarajia kuvitekeleza ili kuboresha huduma ya maji nchini.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni: Kuzuia upotevu wa maji, Kusimamia rasilimali za maji, Kuendeleza rasilimali maji, Kuboresha ubora wa huduma ya maji safi na majitaka, Kusambaza maji mijini na vijijini, Kudhibiti upotevu wa maji, Kujenga uwezo wa kitaasisi wa wizara

Hata hivyo, bado haijabainika moja kwa moja kama vijiji vya Bushola na Lyandu ni miongoni mwa maeneo yatakayopata kipaumbele kupitia bajeti hiyo mpya.

Ni wazi kuwa changamoto ya maji kwa wakazi wa Bushola na Lyandu si jambo la kisiasa, bali ni suala la maisha ya kila siku. Wito umetolewa kwa Wizara ya Maji, SHUWASA, na viongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanashughulikia kwa dharura hali hii ya hatari. Maji ni uhai na hakuna maendeleo bila afya.

MWISHO

Baadhi ya wakazi wa kata ya Mwamalili changamoto ya maji.

Majibu ya SHUWASA

Post a Comment

Previous Post Next Post