Na
Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu
wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amewahimiza wananchi kuendelea
kujiandaa kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu 2025.
Ametoa
wito huo wakati akizungumza kwenye bonanza la michezo la Malula Home Talents
Competition ambalo limefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kitangili,
Manispaa ya Shinyanga, na kwamba amesisitiza umuhimu wa kujiweka tayari na
kupuuza propaganda zisizo na msingi kuhusu uchaguzi huo.
“Uchaguzi
umeelezwa kwenye Katiba ya Tanzania kiasi kwamba hata Rais wa nchi hawezi
kuzuia uchaguzi usifanyike. Sasa kama Rais hawezi, kuna mtu mwingine anaweza?
Hakuna!” amesema Mtatiro kwa msisitizo.
Amesema
baadhi ya vijana wamekuwa wakieneza taarifa za kupotosha kuwa hakutakuwa na
uchaguzi, jambo ambalo si la kweli, kwani uchaguzi ni haki ya kikatiba
inayotekelezwa kila baada ya miaka mitano.
“Tayari
maboresho ya daftari la wapiga kura yamekamilika, vyama mbalimbali vimeshaanza
maandalizi, na kwa upande wa CCM, mgombea urais ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, na
mgombea mwenza ni Balozi Dkt. Nchimbi. Wananchi jiandaeni kushiriki uchaguzi
huu muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Mtatiro ametumia jukwaa hilo kumpongeza mratibu wa bonanza
hilo, Daniesa Malula, kwa juhudi zake katika kuinua vipaji vya vijana kupitia
michezo, akimtaja kuwa ni mfano bora wa vijana wenye maono na uthubutu.
“Vijana
wengi wanapoteza muda kuangalia TV, kubet au kukaa vijiweni bila kazi. Lakini
huyu kijana Malula anajituma kwenye kazi za kijamii. Nakwambia endelea
kupambana, hizi kazi zitakulipa baadaye,” amesema Mtatiro.
Baada
ya kusikiliza changamoto mbalimbali zilizowasilishwa , zikiwemo mahitaji ya
vifaa vya kazi kama kamera ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni mbili,
Mtatiro ameahidi kukutana naye ndani ya wiki mbili ili kumsaidia kupata kiasi
hicho cha fedha.
Post a Comment