" SHINYANGA: SMAUJATA WATOA ELIMU YA KUPINGA UKATILI KWENYE CHUO CHA KIZUMBI

SHINYANGA: SMAUJATA WATOA ELIMU YA KUPINGA UKATILI KWENYE CHUO CHA KIZUMBI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Viongozi wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga wametembelea Chuo cha Kizumbi Institute of Co-operative and Business Education (KICoB) kilichopo chini ya Moshi Co-operative University (MoCU) na kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na uhamasishaji wa haki kwa wote.

Elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi wa chuo hicho kilichopo katika eneo la Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, ambapo viongozi hao wameeleza kuwa vijana ni kundi muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamiri kwenye jamii.

Viongozi wa SMAUJATA akiwemo katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa Bwana Daniel Kapaya, Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mzee Mwarabu Akim wamesisitiza umuhimu wa kila mmoja kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kutoa taarifa za ukatili, kutoa msaada kwa waathirika na kujitokeza kushiriki katika harakati za kuelimisha jamii.

“Ukatili ni adui wa maendeleo, na vijana ndio chachu ya mabadiliko. Tunataka msiwe watazamaji bali muwe sehemu ya suluhisho,.

Pia wameeleza kuwa SMAUJATA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu, serikali na mashirika binafsi ili kuhakikisha ujumbe wa kupinga ukatili unawafikia watu wengi zaidi, hasa maeneo ya mijini na vijijini.

Wanafunzi wa chuo hicho wameeleza kufurahishwa na elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wa kupinga ukatili ndani na nje ya chuo.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post