Na Lydia Lugakila, Misalaba Media - Bukoba.
Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) iliundwa kwa mujibu wa Sheria ya mbegu Na.18 ya mwaka 2003 yenye makao makuu Mkoani Morogoro na Ofisi katika kanda nne nchini, zikijumuisha Kanda ya Ziwa (Mwanza), kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Nyanda za juu Kusini (Njombe) na Kanda ya Kusini (Mtwara).
Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) - Kanda ya Ziwa imefanya mafunzo kwa wafanyabiashara wa mbegu bora kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Kagera mei 29-31, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera lengo likiwa ni kuwajengea uelewa wafanyabiashara wa mbegu bora kuhusu sheria na taratibu zinazosimamia biashara ya mbegu bora.
Wakati wa mafunzo hayo Athuman Fundisha ambaye ni Mkaguzi wa Mbegu kutoka TOSCI- Kanda ya Ziwa alieleza kuwa ili mfanyabiashara aweze kufanya biashara ya mbegu bora ni lazima asajiliwe na TOSCI.
Amesema mafunzo hayo yatawawezesha wafanyabiashara kupata cheti na kibali kitakachoruhusu kufanya biashara hiyo.
Athuman amesema kuwa, ni lazima mfanyabiashara ya mbegu bora apate mafunzo kwa mujibu wa Kanuni za mbegu za mwaka 2007 na atapata cheti cha mafunzo kitakachomwezesha kusajiliwa.
Aliendelea kusema kuwa, ili mfanyabiashara wa mbegu bora aweze kusajiliwa anapaswa kuwa na utambulisho wa mlipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TIN), leseni ya biashara ya pembejeo iliyo hai kutoka mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na cheti cha mafunzo kutoka TOSCI.
"Mfanyabiashara huyo atajisajili na kuomba kibali kupitia mfumo wa kidigiti wa wizara ya Kilimo wa E-Kilimo."akisema Fundisha
Aliongeza kuwa kibali hicho hakina tozo yoyote na kinadumu kwa muda wa miaka 2 ambapo muda wake ukiisha mfanyabiashara atatakiwa kukihuisha.
Amewataka wafanyabiashara kutokuuza mbegu bora kabla ya kusajiliwa na akifanya hivyo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria ya Mbegu na. 18 ya mwaka 2003.
Aidha, Fundisha amesema mfanyabiashara atakayeuza mbegu na kuzichanganya na bidhaa nyingine zisizokuwa pembejeo za kilimo akikamatwa na kukutwa na makosa hayo, atakabiliwa na hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufungwa jela, kulipa faini au vyote kwa pamoja.
"Unakuta kwenye vifaa vya pikipiki na baiskeli wafanyabiashara wanaweka mbegu; hilo ni kosa," alisema Fundisha.
Pamoja na maelezo hayo, Fundisha ametumia fursa hiyo kuwaomba wafanyabiashara wa mbegu bora kuwaelimisha wakulima kwamba mbegu bora za mahindi zote zinauzwa kupitia mfumo wa ruzuku, na pia kuwahamasisha wakulima kufika katika Ofisi za kijiji/mtaa kwa ajili ya kujisajili ili waweze kupata namba za usajili wa mkulima ambayo itawawezesha kununua mbegu hizo kwa bei ya ruzuku.
Ameongeza kuwa kuuza mbegu nje ya mfumo wa ruzuku ni kosa kisheria, kwani Serikali imeamua kutoa ruzuku kwa wakulima ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji hasa kwenye zao la mahindi.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Afisa Kilimo Mkoa wa Kagera, Jackson Mahongo, amewashukuru wauzaji wa mbegu waliojitokeza katika mafunzo hayo kutoka Wilaya za Missenyi, Kyerwa, Ngara, Muleba, Biharamulo, Bukoba Vijijini, Manispaa ya Bukoba, na mikoa jirani.
Mahongo amehimiza umuhimu wa matumizi ya mbegu na miche sahihi, na kusema kuwa wakikosea kwenye mbegu, uzalishaji wa mkulima unashuka.
Amesema kwamba wauzaji wa pembejeo, hasa mbegu bora na miche inayozalishwa kwenye vitalu, ina athari ya moja kwa moja kwa mkulima na Taifa kwa ujumla.
Ameonya kuwa mkulima akitumia miche isiyokuwa na ubora unaotakiwa kisheria, atapata hasara kubwa na kupunguza kipato chake.
"Wewe muuza mbegu ukiuza mbegu za mahindi ambazo hazina ubora, ujue unamuumiza mkulima na Mtanzania kwa ujumla," amesisitiza Mahongo
Amewasisitiza pia wauzaji wa mbegu bora kuuza mbegu sahihi kwa mujibu wa sheria na Miongozo ya Nchi ili kuokoa uchumi wa mkulima.
Aidha, amesema kuwa kuna uhaba wa wauza pembejeo za ruzuku, hasa mbegu za mahindi, na kuwaomba wanakagera kuchangamkia fursa hiyo kwa faida ya wakulima na uchumi wa mkoa.
Bi. Nugwa Fortunatus kutoka TOSCI Makao Makuu yaliyoko Mkoani Morogoro alieleza kuwa uthibiti na udhibiti wa ubora wa mbegu nchini Tanzania unatekelezwa na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) ambapo amesisitiza umuhimu wa wauzaji wa pembejeo katika kusaidia wakulima.
Amebainisha kuwa Maafisa Ugani pekee hawawezi kufanikisha malengo hayo bali juhudi hizo zifanyike kwa ushirikiano wa pamoja wa wadau wote wanaohusika na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.
Aliendelea kusema kuwa TOSCI, inaendeshwa chini ya Wizara ya Kilimo, ilianzishwa ili kuchangia uhakika wa chakula kwa wakulima na Taifa kwa kuhakikisha mbegu bora zinazofikishwa kwa wakulima zinakidhi viwango vya ubora.
Wakizungumza kuhusu manufaa ya mafunzo kutoka TOSCI, Mohamed Said Ally, muuzaji wa mbegu bora kutoka Kabanga, Wilayani Ngara, Mkoani Kagera ameshukuru kwa elimu aliyoipata.
Mohamed Said Ally amesema sasa anaelewa zaidi kuhusu utaratibu wa kupanda mbegu, jinsi ya kukabiliana na magonjwa, na kutafuta vikonya bora wakati wa kupandikiza.
Amesisitiza kuwa elimu hiyo itaboresha ubora wa kazi zao.
Bi. Erika Dario kutoka Kyerwa, Mkoani Kagera, amekiri kupata faida kubwa kutokana na mafunzo hayo, huku akitaja jinsi anavyoweza sasa kuzalisha miche bora ya kahawa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko.
Ameeleza kuwa awali walikosa maarifa kuhusu mbegu zinazoweza kuzalishwa, lakini sasa wanaweza kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora ili kuepuka hasara.
Hata hivyo naye Amos Juma kutoka Nyakanazi wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera, amepongeza TOSCI kwa Elimu ambayo imemsaidia kuelewa uuzaji wa mbegu bora.
Juma amebainisha changamoto ambazo wauzaji hukabiliana nazo, kama mbegu zisizokuwa na ubora ambazo hazioti, hali inayoathiri mazao ya wakulima.
Ameahidi kuendelea kuwauzia wakulima mbegu zilizothibitishwa ubora na TOSCI ili kuleta mafanikio kwa mkulima na Taifa.
Post a Comment