
Waliohama Chadema: Wanakwenda kukifufua Chaumma au kudidimia nacho?
Kuna wimbi la wanasiasa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kukihama chama hicho kikuu cha upinzani na kuhamia chama kingine cha upinzani cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Mei 19, 2025, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe aliwapokea baadhi ya vigogo hao; akiwemo Salum Mwalim ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chaumma, Devotha Minja, Makamu Mwenyekiti Bara na Benson Kigaila, Naibu katibu Mkuu Bara.
Taarifa za vyombo vya habari vya ndani nchini Tanzania zinaeleza, mamia ya wafuasi wengine wa Chadema wako njiani kuhamia Chaumma. Bila shaka hizi ni taarifa za neema kwa chama hicho na taarifa mbaya kwa Chadema.
Mwanasiasa wa ngazi ya juu anapohama chama kimoja kwenda kingine, kuna mambo mawili ya kuyatazama. Je, mafanikio yake ya kisiasa yatakibeba chama anachohamia au mafanikio ya chama hicho yatambeba yeye? Twende polepole, utaelewa.
Katika kesi hii ya vigogo hawa wa zamani wa Chadema – ambao wote watatu wamepata kuwa katika nafasi za juu za uongozi katika chama hicho, inaonekana kwa hakika mafanikio yao kisiasa ni makubwa, kuliko mafanikio ya Chaumma.
Chukua mfano huu: Wakati hayati Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alipohamia chama cha ACT Wazalendo Machi 2019, mafanikio ya Maalim katika siasa yalikuwa ni makubwa kuliko mafanikio ya ACT Wazalendo kwa wakati huo.
Ukubwa wa jina lake, ushawishi na uzoefu, vikaleta neema kwa chama hicho na ghafla kikamea. Kutoka kuwa na Mbunge mmoja baada ya uchaguzi wa 2015 hadi kuwa na Wabunge wanne wa kuchaguliwa baada ya uchaguzi wa 2020.
Wafuasi wa chama wakaongezeka na kujikuta ni sasa ni chama kikuu cha upinzani kwa upande wa Zanzibar. Pia ni sehemu ya serikali ya Umoja wa Kitaifa, kimetoa Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud na kina Mawaziri katika Serikali ya Zanzibar.
Post a Comment