" WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA KAZI ZENYE TIJA ZA MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN – RC MACHA

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA KAZI ZENYE TIJA ZA MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN – RC MACHA



Na. Paul Kasembo – SHY RS.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ametoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga waliohitimu Kidato cha Sita, kuwa mabalozi wa kazi nzuri na zenye manufaa zinazotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maeneo yao ya asili.

Mhe. Macha ametoa wito huo Mei 16, 2025, wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Kidato cha Sita katika shule hiyo, yaliyofanyika katika bwalo la shule na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Shinyanga Mwl. Samson Hango, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Elexius Kagunze, pamoja na wazazi, walezi, wadau wa elimu, walimu na wanafunzi.

Katika hotuba yake, Mhe. Macha alisisitiza kuwa wazazi na walezi wamejionea wenyewe maendeleo makubwa ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na rasilimali watu, ikiwa ni matokeo ya jitihada madhubuti za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Niwaombe wazazi na walezi wote mliohudhuria mahafali haya, muende mkawe mabalozi wa kazi nzuri na zenye tija zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mmejionea maendeleo makubwa ya ujenzi wa shule hii, uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4, ukiwa umekamilika pamoja na vifaa vyake na walimu waliopo,” alisema Mhe. Macha.


Aidha, aliwataka wahitimu kuwa na maadili mema na kujiepusha na tamaa zisizo na tija, huku akiwahimiza kujiandaa ipasavyo kwa masomo ya elimu ya juu.

Akiwasilisha taarifa ya shule, Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Nurah Kamuntu, alisema shule ina jumla ya walimu 23 (16 wa kike na 7 wa kiume), watumishi 9 wasio walimu, wakiwemo matroni 1, mhasibu 1, msanifu wa maabara 1 na mhudumu wa afya 1.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga ni shule ya mchepuo wa Sayansi kwa elimu ya Sekondari ya juu, iliyoanzishwa Agost 13,i 2023 ikiwa na wanafunzi 73 waliomaliza wote kwa mafanikio. Kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 544, wakiwemo 187 wa Kidato cha Kwanza, 127 wa Kidato cha Pili, na 157 wa Kidato cha Tano ambapo Shule inafundisha tahasusi tatu za Sayansi ambazo ni CBG, PCB na PCM.

Post a Comment

Previous Post Next Post