" Waziri Kiongozi Kenya Mudavadi Aunga Mkono Kauli ya Rais Samia Uingiliaji Maswala ya Tanzania

Waziri Kiongozi Kenya Mudavadi Aunga Mkono Kauli ya Rais Samia Uingiliaji Maswala ya Tanzania

 

Musalia Mudavadi Vs Samia
Musalia Mudavadi Vs Samia

Waziri Kiongozi Kenya Mudavadi Aunga Mkono Kauli ya Rais Samia Uingiliaji Maswala ya Tanzania

Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri wa Kenya, Musalia Mudavadi, ameunga mkono hadharani kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuongezeka kwa uingiliaji wa masuala ya ndani ya Tanzania na wanaharakati kutoka nje ya nchi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Citizen TV nchini Kenya mnamo Mei 20, 2025, Mudavadi alisema anaiunga mkono kauli ya Rais Samia kwa sababu ina ukweli ndani yake, hasa kuhusu namna baadhi ya wanaharakati wanavyovuka mipaka ya uhuru wa kujieleza.

“Sitaipinga kwa sababu nadhani kuna ukweli ndani yake. Tukiangalia kile kinachoendelea, kiwango cha matusi na ukosefu wa adabu nchini Kenya umepindukia, ingawa tuna uhuru wa maoni,” alisema Mudavadi wakati akijibu swali la mwandishi Yvonne Okwara kuhusu iwapo Kenya inaweza kuchukua hatua za kidiplomasia kulalamikia kauli ya Samia.

Mudavadi alikiri kuwa changamoto ya ukosefu wa heshima kwenye mijadala ya umma ni jambo linalotokana na uhuru wa maoni usiodhibitiwa vyema.

“Rais Samia anasema watu wanavuka mipaka – huo ni ukweli. Mimi ni Mkenya pia, na namna tunavyoongea, kwa sababu kuna uhuru wa maoni, hakuna heshima,” alisisitiza.

Kauli ya Mudavadi imejiri siku moja baada ya Rais Samia kutoa onyo kali dhidi ya kile alichokiita “wanaharakati wa kigeni” wanaoingilia masuala ya Tanzania.

Akizungumza Mei 19, 2025, Rais Samia alieleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya wanaharakati kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, akitaja juhudi zao kama “majaribio ya kuivuruga Tanzania”.

“Tumeanza kuona mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu, walishaharibu kwao, wasije kutuharibia huku,” alisema Rais Samia huku akiwataka maafisa wa ulinzi na sera za nje kuwa makini.

Kauli hizi zimejiri wakati ambapo wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya walifika nchini Tanzania kufuatilia mwenendo wa kesi ya mwanasiasa Tundu Lissu, hali iliyoibua mjadala mkubwa katika nchi zote mbili.

Wachambuzi wa siasa wanatafsiri matamshi ya viongozi hawa wawili kuwa ni jaribio la kulinda uhuru wa kitaifa na kupunguza ushawishi wa kimataifa usio rasmi katika masuala ya ndani, hasa yanapohusu masuala nyeti ya kisiasa na haki za binadamu.

Post a Comment

Previous Post Next Post