Mdau wa maendeleo mkoani Geita na shabiki wa kikosi cha Yanga, Hussein Makubi Mwananyanzala, amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanikisha ukamilishaji wa Daraja la Magufuli linalounganisha mikoa ya Geita na Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufika na kujionea maendeleo ya daraja hilo, Mwananyanzala amesema ana kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa jitihada kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo daraja hilo ambalo lilihasisiwa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano.
“Nimefika hapa kwa macho yangu na kuona kazi kubwa iliyofanyika. Daraja hili limekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Geita na Mwanza. Ni ishara tosha kuwa Serikali ya Rais Samia inaendeleza kwa vitendo maono ya watangulizi wake kwa maslahi ya Taifa,” alisema Mwananyanzala.
Aidha, aliongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni fursa ya kuimarika kwa uchumi wa wananchi kupitia biashara na huduma mbalimbali za kijamii.
“Miundombinu imara kama hii ni msingi wa maendeleo ya kweli. Tunampongeza Mama Samia si kwa maneno tu bali kwa vitendo – anastahili heshima na kuungwa mkono,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Mwananyanzala, daraja hilo si tu linaboresha maisha ya wananchi, bali linafungua milango ya uwekezaji, utalii na usafiri wa uhakika kati ya mikoa hiyo miwili ya Kanda ya Ziwa.
Post a Comment