Na Elisha Petro Shigera, Misalaba Media Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha watoto wanalelewa na kukua katika misingi bora, hasa wawapo shuleni, ili kuwajengea msingi wa maisha yenye mafanikio.
DC Mtatiro ametoa wito huo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yaliyoenda sambamba na hitimisho la kampeni maalum ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la KKKT Ebeneza, Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mtatiro amesema baadhi ya wazazi na walezi wameanza kusahau misingi ya malezi bora kwa kuruhusu matumizi holela ya simu za mkononi kwa watoto, jambo linalochochea mmomonyoko wa maadili katika jamii.
"Watoto na vijana wengi wanaharibika katika malezi kutokana na uzembe wa wazazi na walezi. Nawaomba watoto mjifunze kuwasikiliza wazazi wenu, na mnapoona jambo la hatari, toeni taarifa haraka. Ukiwa shuleni, ukialikwa sehemu ya hatari, mwambie mwalimu. Kwa upande wa wazazi, tuwe makini na matumizi ya simu kwa watoto; kwa mfano, mtoto wa kidato cha pili au chini yake hana sababu ya kutumia simu kwa siri. Simu imekuwa chanzo cha watoto kushawishiwa vibaya," amesema DC Mtatiro.
Katika hatua nyingine, DC huyo amelipongeza Shirika la Compassion Cluster ya Shinyanga kwa kufanikisha kampeni hiyo na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sheria na sera za kulinda haki za mtoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Watendaji wa Cluster ya Shinyanga ambaye pia ni Mtendaji wa Kituo cha Maendeleo ya Mtoto Ndala, Steven Simon, amesema kampeni hiyo ilianza Mei 10, 2025 katika kituo cha Kitangili, na zaidi ya watu 5,000 wamefikiwa, wakiwemo watoto 2,000.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Kituo cha Polisi Shinyanga Mjini, Inspekta Jene Mwazembe, amewataka washiriki wa maadhimisho hayo kutumia elimu waliyoipata kukabiliana na ukatili na kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii.
Baadhi ya washiriki wa kampeni hiyo wameishukuru Compassion Cluster ya Shinyanga kwa elimu waliyopewa kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni, na kuahidi kuifanyia kazi kwa lengo la kujilinda wao na kuwalinda wenzao.
"Tunashukuru kwa elimu nzuri tuliyoipata kuhusu mimba na ndoa za utotoni. Tumejifunza madhara yake na namna ya kujiepusha nayo. Mkuu wa wilaya ametusihi tuepuke matumizi mabaya ya simu, kwani zinachangia sana kushawishiwa. Tutatumia elimu hii kujilinda sisi na kuwasaidia wenzetu," amesema mmoja wa washiriki.
Post a Comment