Na Lydia Lugakila, Misalaba Media -Karagwe
Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera imepata hati safi huku mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe, Hajjat Fatma Mwassa akiwapongeza watumishi na watendaji wake wa halmashauri hiyo kwa namna walivyopambana hadi kufikia hatua hiyo ambapo amewataka watendaji hao kuendeleza juhudi hizo mwaka hadi mwaka ili kufanya halmashauri hiyo kusonga mbele zaidi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mkaguzi mkuu wa nje Godwin Ibrahim kusoma taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) katika kikao maalum cha Baraza la madiwani.
Ibrahim ameitaja Halmashauri hiyo kupiga hatua nzuri ambayo imetokana na ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya mkoa wa Kagera watendaji wa Halmashauri hiyo wakiwemo madiwani.
"Halmashauri yetu kwa Mwaka 2021 hatukupata hati safi ilikuwa hati isiyoridhisha na baada ya hapo mabadiliko mambo yaliboreshwa ambapo tulibaini kuwa kwa sehemu kubwa ya mabadiliko hayo yalitokana na ushirikiano wa ufanyaji kazi ndani ya halmashauri ya Karagwe" alisema Ibrahim.
Ameipongeza Halmashauri hiyo pamoja na mkuu wa Mkoa huo kwa usimamizi mzuri na uboreshaji wa mazingira kwa watendaji kazi ambapo baada ya hapo zilianza kushuhudiwa kupata hati safi mfululizo hadi sasa.
Mkaguzi huyo ameipongeza Halmashauri hiyo kupata hati safi huku akitoa wito kwa utendaji wake kuendeleza mapambano katika kazi na kuwaomba kuhakikisha uandaaji wao wa mahesabu uwe katika wiwango vinavyohitajika vya mahesabu, na uendane na sheria za mahesabu ili waendelee kuipaisha halmashauri hiyo na mkoa kwa ujumla.
"Hati zipo za aina nyingi ipo hati safi, hati yenye mashaka na hati chafu hivyo tunashukuru Mungu kwani hali hii imetokana na ushirikiano wetu" alisema mkaguzi huyo.
Aidha naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe
Wallece Mashanda amesema kuwa Halmashauri hiyo imepata hati safi iliyotokana na usimamizi mzuri kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Kagera, madiwani mkurugenzi mtendaji pamoja na chama cha mapinduzi CCM ambapo ametoa shukrani kubwa na kuomba jitihadi hizo kuendelea.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika kikao hicho ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe, Hajjat Fatma Mwassa
amesema kuwa kupata hati safi sio kigezo cha kupunguza kasi na badala yake waone haja ya kutumia nguvu zaidi kutimiza majukumu yao ipasavyo ili kwa miaka ijayo hati hiyo iendelee kuwa safi.
Mhe, Mwassa amempongeza Mkurungezi mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na watendaji wote wa Halmashauri hiyo, madiwani kutokana na kazi kubwa ambazo wamekuwa wakifanya juhudi kubwa zilizoleta mafanikio hadi kupata hati safi.
"Nakupongeze pia mkuu wa wilaya, kamati ya usalama ya wilaya pamoja na halmashauri yetu yote kwa juhudi kubwa mlizoweka katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuvuka lengo kwa asilimia 101 ya malengo mliyojiwekea"alisema Mwassa.
Amewahimiza viongozi wa halmashauri hiyo kutoka katika hali ya kubahatisha bahatisha hali inayoweza kusababisha kurudi katika hati yenye mashaka kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma bali hati safi iwe mwendelezo.
Mwassa amesema hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Halmashauri hiyo unaenda vizuri ambapo hadi kufikia mei 31,2025 halmashauri hiyo ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 5.4 sawa na asilimia 101 huku lengo la mwaka likiwa ni bilioni 5.42.
Hata hivyo amesisitiza kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinapelekwa benk sambamba na kuzingatia mfumo wa kukusanyia mapato.
Mkuu wa mkoa huo Ameelekeza Halmashauri hiyo kuhakikisha inakusanya mapato yatokanayo na vyanzo vya ushuru wa mabango na kodi ya majengo, vyanzo vilivyorejesha kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa sasa.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo inapaswa kuongeza mapato yake ili kupata uwezo wa kutekeleza miradi yao pasipo kutegemea kiasi kikubwa fedha kutoka serikali kuu.
Aidha kiongozi huyo amempongeza mkaguzi wa nje kwa namna anavyotoa ushauri, anavyoongoza na ushirikiano mkubwa alioutoa hadi kupatikana kwa hati safi.
Post a Comment