" KYOMBO AACHA HISTORIA KASHENYE KANYIGO NA BWANJAI WAKATI AKITEKELEZA ILANI YA CCM

KYOMBO AACHA HISTORIA KASHENYE KANYIGO NA BWANJAI WAKATI AKITEKELEZA ILANI YA CCM

 
Na Lydia Lugakila 
Missenyi

Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Mhe. Florent Kyombo, amefanya ziara katika kata za Kashenye, Kanyigo, na Bwanjai kuzungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2020–2025 ambapo amepokelewa kwa shangwe kubwa huku wananchi wakionyesha kumuamini kwa makubwa aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano katika uongozi wake.

Wananchi wamejitokeza kwa wingi kumkaribisha huku wakionyesha shukrani kwa maendeleo yaliyotekelezwa, ikiwa ni pamoja na miradi ya maji, shule, afya, na Barabara.

Katika mkutano huo, Mhe. Kyombo ameeleza hatua kwa hatua maendeleo ambayo yamefanyika na yanayoendelea kufanyika kwa sasa.

Wananchi walionyesha kuridhika na kazi za mbunge huyo, huku wakimpa heshima ya kumuamini na kumuomba mwenyezi Mungu aweze kumuweka tena madarakani kiongozi huyo muda ukiwadia.

Wananchi hao pia wamemzungumzia Mhe Kyombo kama kiongozi anayeishi kwa vitendo.

Mhe. Kyombo amezungumza kuhusu umuhimu wa uongozi bora, utu, na uaminifu katika kuwahudumia wananchi, huku akiwahimiza wananchi kuchagua viongozi wenye maono na ambao wanajali na kutatua changamoto zao.

Wananchi walimpongeza kwa kazi nzuri na mafanikio katika sekta mbalimbali hususan katika maji na afya huku wakionyesha matumaini ya kuona mabadiliko chanya kupitia viongozi watiifu kama mbunge huyo.

Ikumbukwe kuwa bunge wa Jimbo la Missenyi mkoani Kagera Mhe. Florent Kyombo, amefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya jimbo ilo zikiwemo kata za Bwanjai, Kashenye  na Kanyigo lengo likiwa ni kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano.

Katika mikutano hiyo pia Mhe. Kyombo ameeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji safi, na nishati vijijini, akisema kuwa hatua hiyo imechochea ustawi wa maisha ya wananchi wa Missenyi.

Akiwahutubia wananchi kwa nyakati tofauti, Mhe. Kyombo ameongeza kuwa ameleta mapinduzi makubwa katika Jimbo hilo na kuonyesha uongozi uliotukuka na kulisemea Jimbo hilo kila mara anapopata nafasi  bungeni.

"Uongozi bora na utu, uaminifu, na uadilifu vinatakiwa katika safari ya kuwahudumia wananchi na ndio maana umeona mimi Kyombo leo hii bado nakubalika kwa wananchi wangu"alisema mbunge huyo.

“Tumeona viongozi wengi wenye uwezo wa kifedha lakini hawana nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi  naomba tuendelee kuchagua viongozi  wenye maono watakaoleta maendeleo katika eneo husika na watakaoshughulika na changamoto za Wananchi"alisema  Kyombo.

Aidha Wananchi walioshiriki mikutano hiyo  akiwemo Jasintha Martin kutoka Kanyigo, Joel Kabate na Johansen Kaiza wamempongeza mbunge huyo kwa uongozi wake imara na kuongeza kuwa miradi mingi imeonekana kwa vitendo na si maneno hususani katika sekta ya maji na afya.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Mhe. Kyombo kuendeleza ushirikiano na wananchi huku akiwa katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Hata hivyo wananchi hao wamesema wanatarajia uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa wa amani  huku wakiwa na nguvu ya kuwa sehemu ya  kufanya maamuzi sahihi ili kuwapata viongozi sahihi.
















Post a Comment

Previous Post Next Post