Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, chama hicho kinaendelea na maandalizi ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wanachama watakaowania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia CCM.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato huo utafanyika kwa hatua, ikiwemo uchukuaji na urejeshaji wa fomu, vikao vya awali na hatimaye kura za maoni. Hivyo, chama kimeagiza kusitishwa kwa shughuli zozote zinazohusiana na vikao vya uteuzi kabla ya hatua ya kura za maoni.
"Ni kwa kuzingatia hilo, CCM inasisitiza marufuku ya ZIARA, MIKUTANO, SEMINA na MAKONGAMANO yanayohusisha wajumbe wa vikao vinavyopiga kura za maoni kuhusiana na wagombea wa ngazi zote hadi kura za maoni zitakapopigwa," imesisitizwa kwenye taarifa hiyo.
Aidha, CCM imeonya wanachama wote wanaotarajia kugombea au wawakilishi wao dhidi ya kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kuashiria ukiukwaji wa Katiba, kanuni au miongozo ya chama hicho.
Chama hicho pia kimewataka viongozi, watendaji na wanachama wake kusimamia nidhamu, maadili na mshikamano katika kipindi hiki muhimu cha maandalizi ya uchaguzi. Viongozi wote wametakiwa kuhakikisha kuwa michakato yote inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amehitimisha taarifa hiyo kwa kuwataka wanachama wote kutimiza wajibu wao katika kuimarisha umoja ndani ya chama na kudumisha imani ya wananchi waliyopewa na CCM.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!

Post a Comment