
Na Mwandishi Wetu, Misalaba Media
Ikiwa imebaki miezi michache tu kufanya uchaguzi mkuu, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi na kuboresha huduma za kijamii nchini. Katika yote haya, imekuwa nyota inayong’aa si tu kwa Afrika Mashariki, bali pia kwa Bara la Afrika kwa jumla.
Utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii umefanyika kwa kuongozwa na sera, sheria, kanuni, taratibu na utekelezaji wa mikakati mbalimbali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo endelevu.
Dkt Samia Suluhu Hassan alianzisha ajenda ya ‘4R’ kama nguzo muhimu ya maendeleo inayolenga maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya mustakabali wa kitaifa kisiasa. Lengo ni kuboresha mahusiano kitaifa, kikanda na kimataifa, na kuhakikisha tunajenga taswira mpya ya Tanzania, huku tukiendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi.
Alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021, Dkt Samia Suluhu Hassan aliahidi kuimarisha demokrasia, haki za binadamu, kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ya maji, kuboresha usafiri wa umma na usafirishaji wa mizigo, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na mahusiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa, na kuendeleza mazuri ya awamu zilizopita, ikiwa ni pamoja na kuleta mambo mapya, yanayoendana na wakati tuliomo.
Ukuaji wa Uchumi
Serikali yoyote duniani katika ukusaji wa mapato ili kuimarisha uchumi wa ndani inategemea usimamiaji madhubuti wa sera, programu na mikakati mbalimbali kwa kuhakikisha mapato yanazidi kukua siku hadi siku. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21, serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi trilioni 20.59 na katika mwaka wa fedha 2023/24, ilikusanya kiasi cha Shilingi trillioni 28.83, ambazo ni mapato ya ndani. Pamoja na mambo mengine, katika ukusanyaji wa mapato, Shilingi trilioni 120.16 zilikusanywa kutoka vyanzo vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wizara, wakala wa serikali na serikali za mitaa.
Elimu
Katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu, serikali ya awamu ya sita iliamua kuondoa ada, na ilianza kusambaza vitabu, na kujenga madarasa, na pamoja na mambo mengine kufanya mapitio ya Sera ya Elimu, mafunzo ya ufundi na mitaala ili kuhakikisha wahitimu wanapata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Katika sekta ya elimu, ambapo mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) yanalenga kuhakikisha wahitimu wanakuwa na maarifa, ujuzi, na maadili ili waweze kupenya katika soko la ajira.
Serikali iliamua kujenga shule 26 za wasichana za masomo ya sayansi kila mkoa, na shule 7 za wavulana kila kata nchi nzima, shule za msingi na sekondari 191,708 zilijengwa hadi mwaka 2020, na shule 254, 393 zimejengwa nchi nzima hadi mwaka 2025.
Pamoja na mambo mengine, shule za msingi mpya zilizojengwa mwaka 2025 ni 17, 986 na hadi mwaka 2020 zilizokuwepo shule 16,406. Idadi ya shule zote hizi ni matokeo chanya ya Ilani ya CCM.
Vile vile serikali iliongeza vyuo vya ufundi stadi kutoka vyuo 662 mwaka 2020 hadi vyuo 860 mwaka 2024 kuendeleza ujuzi wa Watanzania katika sekta ya ufundi.
Afya
Msingi wa maendeleo ni pamoja na kuboresha afya ya umma. Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan iliwekeza katika sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya afya kutoka 8,783 mwaka 2020 hadi vituo vya afya 12, 846, na kuboresha miundombinu ya majengo, kununua vifaa tiba, kuboresha huduma za kibingwa na kusomesha madaktari na wahudumu wengine katika sekta ya afya.
“Miaka minne iliyopita idadi ya vifo vya akina mama wanaojifungua ilikuwa 556 kati ya 100,000, lakini kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, idadi ya vifo ilipungua hadi kufikia 104. Lengo la dunia ni vifo 70. Nina hakika tutafika huko na kuondoa kabisa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” alisema Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya mojawapo nchini.
Maji
Miaka michache iliyopita akina mama walikuwa wakiamka alfajiri na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo pia walikuwa hawana uhakika kama wangeweza kuyapata. Hadi kufikia mwaka huu, serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi ya usambazaji wa maji 2,331 katika miji na vijiji. Miongoni mwa miradi hiyo, ni ile ya Same, Mwanga na Korogwe ambapo wananchi wapatao 456,930 wamenufaika na miradi ya maji safi na salama.
Kilimo
Kwa miaka mingi kumekuwa na kauli mbiu mbalimbali za uhamasishaji wa kilimo tangu serikali ya awamu ya kwanza kama vile siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, na kilimo kwanza (ambayo ilikuwa kauli mbiu ya serikali ya awamu ya nne). Kilimo ni uti wa mgongo, na kauli mbiu hii inathibitisha utekelezaji wa sera ya kilimo kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza bajeti yake kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi Shilingi trilioni 1.24 mwaka 2024/25, na kuifanya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 26.2 kwa pato la taifa
Miaka ya nyuma Tanzania ilitofautisha mazao ya chakula, na ya biashara, lakini kwa sasa mazao karibu yote ni ya biashara, na mahitaji ni makubwa kwenye soko la nje, hata nyama kutoka Tanzania ambayo ni fursa muhimu kwa wakulima na wafugaji, lakini pamoja na mambo mengine, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17.1 mwaka 2021 hadi tani million 22.8 mwaka 2024, huku serikali ikitoa ruzuku ya Shilingi billioni 300 katika kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo huajiri takribani asilimia 65 ya nguvu kazi.
Mifugo na Uvuvi
Serikali ya awamu ya sita imbadilisha mfumo wa kizamani na kuweka mfumo wa kisasa kuhakikisha ajira za Watanzania zinaendelea kuongezeka na usalama wa chakula una kuwa wa uhakika kwa kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo kutoka tani millioni 1.38 mwaka 2020 hadi tani millioni 2.6 mwaka 2025, na kuongeza maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta millioni 2.78 hadi hekta millioni 3.48. Ongezeko hili limepunguza migogoro ya wakulima na wafugaji, huku mauzo ya nyama nje ya nchi yakiongezeka pia kutoka tani 1,774 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 4.2 mwaka 2020 hadi tani 9,863.41 zenye thamani ya Dola za Kimarekani (USD) millioni 44 mwaka 2025.
Madini
Sekta ya madini kwa muda mrefu ilionekana kama urithi wenye laana, lakini kwa sasa sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa imeboreshwa kupitia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2019, na mwaka 2022 mchango wake katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10.1 mwaka 2025. Masoko ya madini yameongezeka kutoka 41 mwaka 2021 hadi kufikia 43 mwaka 2025 na vituo vya madini vimeongezeka kutoka 61 hadi kufikia vituo 109. Uboreshaji katika sekta ya madini umesogeza huduma kwa wananchi, na kuongeza uwazi katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Katika kuhakikisha mchango wa sekta hii unaendelea kukua kwa kasi, serikali ya awamu ya sita iliamua kununua mitambo 15 ya uchongoraji kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisambaza sehemu mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na kupanua uwazi wa sekta ya madini.
Pamoja na mambo mengine, baada ya kilio hicho cha muda mrefu na baadaye kwa kuwa na Sera ya Madini ya mwaka 2009 ya kuwawezesha Watanzania wazawa kushiriki katika sekta ya uchimbaji wa madini, kupata kazi za ukandarasi, zabuni na kutoa huduma mbalimbali kupitia Kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content) Watanzania wamekuwa wakipata ajira ndani ya migodi na nafasi za menejimenti kushikwa na wazawa.
Kwa sasa serikali iko mbioni kujenga kituo cha kisasa cha maabara kwa ajili ya upimaji wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo ipo jijini Dodoma. Katika kipindi cha miaka minne ya awamu ya sita, chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan, serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kwa kutoa fursa kwa wazawa katika sekta ya madini kwa upatikanaji wa kazi migodini na marekebisho ya Uwajibikaji wa Jamii (CSR).
Viwanda
Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kijani kupitia viwanda, na kupunguza tatizo la ajira nchini kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya viwanda 47,063 vilianzishwa. Kati ya hivyo, viwanda vikubwa ni 428, vya kati ni 1,393, vidogo ni 11,847 na vidogo sana ni 33,395, na pamoja na mambo mengine, kuendeleza kiwanda cha ngozi (Kilimanjaro Leather International Company Limited) kinachomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa asilimia 86, na Jeshi la Magereza kwa asilimia 14 kwa uwekezaji wa Shilingi billioni 152.96. Kwa hakika sekta ya viwanda ni injini kwa maendeleo ya taifa.
Makala haya hayawezi kutosha kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameisimamia kikamilifu ili kulinda na kuendeleza maliasili na utalii, uchukuzi, miundombinu, ardhi, nishati, mawasiliano na sekta zingine mtambuka kwa masilahi mapana ya nchini yetu.





Post a Comment