

Na Mapuli Kitina Misalaba
Katika harakati za kuhamasisha jamii kuhusu kupinga ukatili na kuchagua
viongozi bora kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na
Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga imehudhuria semina
maalumu katika Kanisa la RAGT lililopo Kitangili Manispaa ya Shinyanga, ambapo
waumini wamepata nafasi ya kufundishwa masuala ya maadili, haki, na ustawi wa
familia.
Akizungumza katika semina hiyo, Makamu Mwenyekiti wa
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwarabu
Akim ametoa wito kwa wananchi na waumini kutokubali kununuliwa kwa pesa
au zawadi katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi wa 2025.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa taifa
letu. Tuchague kwa busara. Tusikubali kiongozi anayekuja na rushwa ya hela au
vitenge atupumbaze. Huyo akishinda, hatakuwa na uchungu na sisi. Atakuwa
anaangalia namna ya kurudisha alichotumia badala ya kutatua changamoto zetu,”
amesema Mwarabu.
Mwarabu amesisitiza kuwa upigaji kura siyo tukio la
kawaida bali ni uamuzi wa miaka mitano wa maendeleo au kurudi nyuma kwa jamii.
“Huu siyo wakati wa mihemko wala ugomvi. Uchaguzi si
vita, ni nafasi ya kuchagua kwa akili. Tusikilize hoja za wagombea, si misuli
au maneno matamu ya kununua dhamira zetu,” ameongeza.
Katika mjadala huo wa semina, Mwarabu pia ametoa elimu
kuhusu aina mbalimbali za ukatili unaoitesa jamii, ikiwemo ukatili wa kimwili,
kingono, kisaikolojia, na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Meryester Nyalusanda
amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema, akisisitiza
kwamba matumizi ya maneno mabaya na adhabu zisizo na busara kwa watoto hujenga
kizazi kilichovunjika kisaikolojia.
“Watoto
ni kioo cha familia. Wakiwa wameharibika ni jamii yote imeharibika. Tuwape
maneno ya matumaini na siyo ya kuwadhalilisha. Tuwaadhibu kwa hekima pale
wanapokosea ili kuwajenga, si kuwavunja moyo,”
amesema.
Nyalusanda pia ametumia nafasi hiyo kukemea tabia ya
baadhi ya wanawake walokole kuwadharau waume zao kwa kisingizio cha kuwa
"wameokoka".
“Wanawake
tumekuwa na changamoto moja, hasa sisi walokole. Tumekuwa na tabia ya kuwa bize
na maombi, kiasi kwamba baadhi ya wanawake wakishaingia rohoni, wanasahau
kwamba baba (mume) naye anahitaji huduma”.
“Kuna
wakati mume wako anakuhitaji apate haki yake ya msingi ya ndoa kwa wakati
sahihi, lakini badala ya kumjali, unamuita pepo. Unamtamkia: 'We popo, hujui kama nimefunga?'
Wakati maandiko yanasema kabla ya jambo lolote, mshauriane na muelewane”.
“Inamaanisha
kwamba kabla hujafunga, unatakiwa kumshirikisha mume wako mapema ili ajue,
kuliko kumkurupusha. Haya mambo ndiyo yanasababisha ndoa nyingi kuyumba na
kuharibika”.
“Tumeokoka,
lakini ndoa zetu zina migogoro. Siri ni nini?, Ni kwa sababu wanawake
tunajiweka kama vile tumekuwa watakatifu kuliko waume zetu”.
“Ukumbuke
kwamba kabla ya kwenda kanisani, mume wako ni muhimu sana kuliko hata mtumishi
wa Mungu au baba yako wa kiroho, kwa hiyo wanawake tubadilike. Tuwe mfano mwema
katika jamii.”
Makamu Mwenyekiti wa
SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Kabizi Gombo, ameeleza kuwa watoto
wengi wanakumbwa na ukatili wa kunyimwa haki zao za msingi kama elimu, chakula,
na malezi bora, akisema ni wajibu wa jamii kuhakikisha mtoto analelewa kwa
upendo na si kwa manyanyaso.
Naye Katibu
wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Husna Maige, amesema SMAUJATA ipo kwa
ajili ya kupaza sauti dhidi ya ukatili wa aina yoyote mahali popote.
“Malengo yetu ni kuhakikisha kila sauti ya mnyonge
inasikika. Tunasimama na kila mmoja anayepitia ukatili. Hatutafumbia macho
vitendo vinavyohatarisha ustawi wa jamii,” amesema Husna.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Makundi Maalum wa SMAUJATA Manispaa
ya Shinyanga, Leokadia Daudi, amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele
katika kutetea amani ya ndoa kwa kuepuka vitendo vya ukatili dhidi ya waume
zao, ikiwemo kuwakosesha heshima na haki zao.
“Wanawake tukitaka ndoa zetu zidumu, lazima turejee
kwenye heshima, utiifu na mawasiliano yenye hekima. Kuolewa si kufungwa, bali
ni kushirikiana kwa upendo na maelewano.”
Kwa upande wake, Askofu Jacob Sallu wa Kanisa hilo la
RAGT amewapongeza viongozi wa SMAUJATA kwa kufikisha ujumbe muhimu wa kupinga
ukatili, huku akiwahimiza waumini kuwa mabalozi wa amani na maadili mema katika
familia zao.
Naye Askofu Enock Ndezi wa Kanisa la RAGT kutoka Dar
es Salaam, amepongeza juhudi zinazofanywa na viongozi wa SMAUJATA kwa kuwafikia
waumini kwa elimu yenye kujenga na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii.
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwarabu Akim akizungumza kwenye
semina katika kanisa la RAGT Kitangili Manispaa ya Shinyanga.

Askofu Jacob Sallu wa Kanisa hilo la RAGT, akitoa
mahubiri yake.
Mwenyekiti wa SMAUJATA
Manispaa ya Shinyanga, Meryester Nyalusanda, akitoa elimu ya
masuala ya ukatili katika kanisa la RAGT lililopo Kitangili mjini Shinyanga.

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Kabizi Gombo, akitoa elimu ya ukatili hasa kwa watoto kuhakikisha wanapata haki zao.




Askofu Enock Ndezi wa Kanisa la RAGT kutoka Dar es Salaam, akihubiri katika semina hiyo.


Mwenyekiti wa Idara ya
Wanawake na Makundi Maalum wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Leokadia Daudi,
akizungumza kwenye semina hiyo.


Post a Comment