
KUNDI la fisi limevamia nyumbani kwa mkazi wa Kijiji cha Gambasingu, Kata ya Nkoma, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Singisi Kija na kuua kondoo 17 na mbuzi watano.
Aidha fisi hao walijeruhi mbuzi wawili na kondoo watatu Agosti 20, mwaka huu saa 6:25 usiku.
Singisi aliwaeleza waandishi wa habari nyumba kwake kuwa alianza kusikia sauti za mbuzi wakipiga kelele sana saa sita usiku na alikwenda kuangalia.
Alisema alikuta kundi la fisi wanne wakiwa ndani ya zizi la mifugo hiyo na alipiga kelele kuomba msaada kutoka kwa majirani.
“Wale fisi wakakimbia na majirani walianza kufika na tukaanza kuwakimbiza na kutokomea vichakani ndipo tukarudi kuangalia kwenye zizi na kukuta madhara hayo,” alisema Singisi.
Alisema tukio hilo si mara ya kwanza kwake kwani wamewahi kufanya hivyo mara mbili na mara ya kwanza walivamia na kuua kondoo na mbuzi 25 na mara ya pili waliua mbuzi watano.
Lucas Kikaja mmoja wa majirani aliyeshuhudia tukio hilo, alisema kuwa baada ya kusikia kelele alifika nyumbani kwa Singisi na kuanza kuwakimbiza fisi hao ambao walifanikiwa kutokemea kwenye vichaka.
“Baada ya kuwakimbiza tulirudi kuangalia kwenye zizi, tulikuta wamefanya uharibifu mkubwa, tulikuta mbuzi watano wamekufa, kondoo 17 nao wamekufa huku wengine kondoo na mbuzi wakiwa wamejeruhiwa,” alisema Kikaja.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Buka Bulugu alikiri kutokea kwa tukio hilo, huku akibainisha kuwa walitoa taarifa ofisi za maliasili wilaya ambao walifika na kuchukua taarifa mbalimbali.
Bulugu alieleza kuwa alikuwa mtu wa pili kufika kwenye tukio hilo majira ya usiku na aliwashuhudia fisi hao wakiwa wanne wakati wanawakimbiza, huku akiomba serikali kusaidia kumlipa fidia mwananchi huyo.
“Tunaiomba serikali kumsaidia kupata fidia mwananchi huyo kwani amepata hasara kubwa sana na mifugo hao ndiyo ilikuwa tegemeo kubwa sana kwake katika kuendesha maisha na familia yake,” alisema Bulugu.
Hata hivyo wananchi wa kijiji hicho waliomba waondolewe kwa wanyamapori hao kwani wamekuwa kero kubwa kwa kuvamia na kuua mifugo yao mara kwa mara.
Post a Comment