" Naibu Waziri Mkuu kuzindua teknolojia ya kuondoa uvimbe bila upasuaji

Naibu Waziri Mkuu kuzindua teknolojia ya kuondoa uvimbe bila upasuaji

 Mwandishi Wetu


NAIBU Waziri Mkuu, Dotto Biteko anatarajiwa kuzindua teknolojia mpya ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayofahamika kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU).

Uzinduzi wa teknolojia hiyo utafanyika tarehe 26 mwezi huu kwenye hospitali ya Kairuki Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kauriki Hospital, Dk Onesmo Kaganda wakati akizungumzia uzinduzi huo.

Alisema uzinduzi wa HIFU ni tukio la kihistoria kwakuwa ni mara ya kwanza katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati huduma hii inazinduliwa.

Alisema kabla ya kuingia hapa Tanzania, teknolojia hiyo imeanzishwa katika nchi tatu tu za barani Afrika ikiwemo Misri, Nigeria na Afrika Kusini.

Alisema HIFU ni Teknolojia ya kisasa inayotumia Mawimbi Sauti (Sound Waves) kutibu aina mbalimbali za uvimbe mwilini bila upasuaji, ikiwemo uvimbe wa saratani na usiokuwa wa saratani katika maeneo kama Matiti, Kongosho, Kizazi kwa Wanawake, na Tezi Dume kwa wanaume.

Alitaja faida za huduma hiyo kuwa ni pamoja na mgonjwa kutolazimika kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe.

Alisema hakuna kovu kwa kuwa hakuna upasuaji na mgonjwa hupona kwa muda mfupi na kurejea katika shughuli zake za kila siku kwa haraka.

Dk Kaganda alisema matibabu haya hayahitaji kumwongezea damu mgonjwa hata kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu na kwamba kupatikana kwa huduma hiyo hapa nchini kunapunguza gharama za kwenda nje ya nchi.

“Faida nyingine ya HIFU ni pamoja na tiba shufaa kusaidia dawa za saratani kufanyakazi vizuri mwilini kufubaza kukua kwa saratani mwilini (slowdown disease progression) na kupunguza maumivu kwa wagonjwa wa saratani,” alisema

“Mtambo huu unaitambulisha Tanzania kama nchi ya kwanza Afrika Mashariki na kati katika ukuaji wa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma za afya,” alisema.




Post a Comment

Previous Post Next Post