" NIFFER AFUNGULIWA KESI YA BIL.2 MAHAKAMA KUU, KISA KASHFA MTANDAONI

NIFFER AFUNGULIWA KESI YA BIL.2 MAHAKAMA KUU, KISA KASHFA MTANDAONI

 MFANYABIASHARA maarufu wa chakula na vipodozi jijini Mbeya, Mariam Enzi amefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Mbeya dhidi ya mfanyabiashara, Jenifer Jovin Bilikwija maarufu kama ‘Niffer’ akimdai fidia ya zaidi ya Shilingi Bilioni mbili kwa madai ya kashfa na usumbufu wa kibiashara.


Kesi hiyo ya madai ni namba 50578 ya mwaka 2025, imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Victoria Nongwa na itatajwa kwa mara ya kwanza Agosti 26, 2025.

Kwa mujibu wa hati ya madai aliyoiwasilisha kupitia Wakili wake, Faraja Msuya wa kampuni ya Client Shield Advocates, Mariam anadai kwamba Julai 4, 2025, aliingia makubaliano ya kibiashara na Jenifer kwa ajili ya kununua vipodozi vyenye thamani ya shilingi milioni 4.682.

Fedha hizo zililipwa kupitia akaunti ya mume wa Mariam, lakini baada ya kupeleka uthibitisho wa malipo, Jenifer alikaa kimya kwa zaidi ya wiki moja. Mariam alipoamua kufika binafsi katika duka la Jenifer lililopo Sinza Kumekucha, hakumkuta, bali jioni yake alipigiwa simu na kutukanwa kwa madai kuwa ametuma risiti feki ya benki.

Aidha, Mariam anadai kuwa Jenifer aliweka taarifa hizo kwenye ukurasa wake wa Instagram, akimtuhumu hadharani kuwa tapeli na mwizi, na kuchapisha risiti husika pamoja na maneno ya kejeli. Baadaye, taarifa hizo ziliripotiwa hadi benki wanayotumia Mariam na mume wake, hali ambayo imesababisha kupoteza imani ya wadau na wateja wake.

“Kitendo hicho kimeniharibia heshima, kimeniacha kwenye fedheha kubwa na kuniharibia biashara zangu kabisa,” Mariam amesema katika hati ya madai.

Katika madai yaliyopo mahakamani, Mariam anaiomba Mahakama imwamuru Jenifer, alimpe fidia mahsusi ya shilingi bilioni 2, kisha arejeshe shilingi milioni 4.682 alizolipa pamoja na riba ya asilimia 30.

Mbali na hilo pia amlipe fidia ya jumla, gharama za kuendesha kesi na riba za kisheria hadi malipo kamili.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post