" PASIPOTI UFUNGUO PEKEE WA KUKUFUNGULIA DUNIA

PASIPOTI UFUNGUO PEKEE WA KUKUFUNGULIA DUNIA







Na Gideon Gregory, Dodoma

Katika dunia ya leo, fursa za elimu, ajira na biashara hufunguliwa zaidi na mipaka ya kimataifa, ambapo ufunguo pekee ni kuwa na pasipoti ambayo ndiyo tiketi ya kwanza ya kukufikisha huko, Bila pasipoti, ndoto zako za kuvuka mipaka zinaweza kubaki hadithi tu.

Kwa mujibu wa mamlaka za uhamiaji kupitia Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Isaac Maganga anawahimizwa wananchi kuomba pasipoti mapema bila kusubiri dharura, ili kuepuka kupoteza nafasi zinazoweza kubadilisha maisha yao.

“Mwananchi anapaswa kuwa na pasipoti muda wowote ule, asisubilie dharura kwamba kwasasa nimepata safari ngoja nikatafute pasipoti, unaweza kukutana na changamoto nyingine ambayo ikakuchelewesha na safari yako.
Kwamba safari yako ipo ndani ya siku mbili, nasisi utoaji wa huduma yetu ya pasipoti sana sana kwa upande wa mikoani huwa inaenda hatua kwa hatua kwani mpaka tupeleke ofisi za printingi Dar es Salaam kwahiyo kama una dharura ndani ya siku mbili hautaweza kuipata kwa uharaka sana kiasi hicho,”amesema.

Anasema kutokana na elimu wanayoendelea kuitoa muamko wa wananchi kupata pasipoti umeongezeka matharani ndani ya Mkoa wa Dodoma ambapo kwa siku wanapata maombi zaidi ya 20.

Aidha, Bwana Maganga anawahimiza wananchi na vijana kutoisubiri dharura bali kuomba pasipoti mapema ili kwenda kutimiza ndoto zao za kufanya kazi na kuizunguka dunia.

“Tusijifunge tu ufahamu wetu wa kubaki Tanzania tu na kutafuta ajira Tanzania tu peke yake, tushapata elimu Serikali inatusaidia tuna elimu za kutosha, kwahiyo pasipoti ndiyo hati pekee inayokufanya wewe kukuunganisha na dunia,”anahimiza.

Anaongeza kuwa licha pasipoti kuwa muhimu, lakini kama mtu hauna ndoto ya kusafiri nje ya nchi Pasipoti sio lazima kwako, japo inaweza kutumika kama kitambulisho ukiwa nje ya nchi lakini ukiwa ndani ya nchi haitumiki kama kitambulisho kwasababu unaweza kuichukua ukabaki nayo ndani kama maktaba yako binafsi ndani.

Je, utaratibu wa kupata ukoje?

Bwana Maganga anasema utaratibu wa kupata Pasipoti ni rahisi, wanaangalia kwanza lazima uwe na shughuli maalum ya kufanya kwasababu hawawezi kutoa pasipoti kwa mtu yeyote ambaye haeleweki anafanya shughuli gani halali.

“Kwa maana hiyo tuna maanisha kwamba mfanyabiashara ana vitu vya kuwasilisha ili aweze kupata pasipoti, lazima tupitie leseni yake ya kibiashara ambayo iko hai na Tin namba kwahiyo tunatambua huyu shughuli yake ni mfanyabiashara kweli lakini pia kwa watumishi wa umma tunapokea barua kutoka kwa mwajili wake,”anasema.

Anasema wanafanya hivyo ni kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kwani mwingine unakuta anakuja kuchukua pasipoti afanyi biashara halali, mwingine anajishughulisha na biashara haramu ambapo ikitokea mtu wa hivyo amekamatwa nje ya nchi anachafua picha ya nchi.

“Kesi za namna hiyo zipo nyingi kwa mfano mwaka jana kuna watu walitangazwa kwenye vyombo vya habari walifanyiwa utaratibu na maajenti ambao sijui walitokea wapi, wakafanyiwa utaratibu wakapata pasipoti lakini wahusika wenyewe wametafutiwa pasipoti na hawajui wanapelekwa wapi ila waliambiwa tu kuna kibarua kimetokea sehemu malipo ni mazuri wakawa wamepelekwa nje mwisho wa siku wakajikuta wako kwenye madanguro,”anasema.

Anaongeza kuwa kwa tukio kama hilo linawapa taswira kwamba kwenye vigezo na masharti lazima wavizingatie, pasipoti ni haki ya kila mtanzania lakini kigezo na sharti lazima vizingatiwe kama haueleweki unafanya shughuli gani hatuwezi kukupa pasipoti ya Tanzania maana hatujui unaenda kuitumia kwa matumizi gani na Serikali inaingia gharama kubwa katika kuzitengeneza.

Sambamba na hayo anawahimiza waombaji kuhakikisha wanapoomba pasipoti wanaifanyia shughuli halali japo hupangiwi matumizi ila yatakuweka katika hali ya usalama na hautosumbuliwa hata ukiwa katika mataifa mengine nje ya Tanzania.

“Kuna wengine wanakuwa wanachukua pasipoti, wanatupa taarifa hizi ila mwisho wa siku wakifika huko nje ya nchi wanaenda kujihusisha mfano na biashara haramu, “anasema.

Ili kutambua changamoto zipi zinazowakabili watu wakati wa kuomba pasipoti nimezungumza na Esther (Jina sio rasmi), moja kati vijana waliowahi kuomba pasipoti kwaajili ya kwenda nje ya nchi ambaye hapa anatueleza

“Changamoto ni kwa watoto wanapokuwa sasahivi, kwa mfano unakuta mzazi chimbuko lake ni Msukuma halafu mtoto amezaliwa Dodoma hajui kisukuma akienda kuomba pasipoti pale kwa Migration officer anamwambia ili niamini kweli wewe ni msukuma hemu tuongee kisukuma na unakuta mtoto hakijui na labda mzazi wake naye hakijui kwahiyo mpaka amtafute mtu mwingine anayemjua ili amtambulishe au alete vitambulisho, kwahiyo hiyo ni moja kati ya changamoto kubwa,”anasema

Esther anasema kusubiri dharura kabla ya kuomba pasipoti ni kujinyima fursa, kwani ni nyaraka ya uhakika wa safari, ulinzi wa uraia wako, na daraja la kukufikisha kwenye ndoto zako za kimataifa.

“Sasa hivi sisi vijana tuna nafasi kubwa ndani na nje ya nchi, kwahiyo kama tunavyoomba namba ya nida ndivyo tunapaswa kuwa na pasipoti hivyo tunapaswa kuwa nayo ili fursa zinapokuja zisitukimbie,”anasema.

Bwana Maganga anasema Pasipoti ni hati ya safari ambayo anapewa mwananchi Mtanzania ili aweze kusafiri nje ya nchi kwa matumizi ya safari nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali ikiwemo vikao na kibiashara.

Post a Comment

Previous Post Next Post