" TAMASHA LA UTAMADUNI JIGOKU MASWA: CHIFU ANTONIA SANGALALI KUFANYA ZIARA NCHI NZIMA KUMUOMBEA KURA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN

TAMASHA LA UTAMADUNI JIGOKU MASWA: CHIFU ANTONIA SANGALALI KUFANYA ZIARA NCHI NZIMA KUMUOMBEA KURA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Machifu Tanzania ambaye ni Ntemi wa Himaya ya Jigoku (Masela) iliyopo Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, Chifu Antonia Sangalali, ametangaza kufanya ziara katika kila mkoa nchini kwa ajili ya kumuombea kura mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza Agosti 24, 2025 katika tamasha lake la utamaduni linalofanyika kila mwaka kwa lengo la kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa kabila la Wasukuma, Chifu Antonia amesema dhamira yake ni kuhimiza wananchi kote nchini kumpigia kura za ndiyo Mhe. Samia kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Amesema katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia amefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya, ujenzi wa miundombinu, madaraja pamoja na sekta nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Chifu Antonia ameongeza kuwa yeye pamoja na Machifu wengine nchini wataendelea kumuunga mkono Rais Samia huku wakihamasisha wananchi kila kona kuhakikisha wanashiriki uchaguzi na kumpigia kura kwa wingi.

“Tutaenda mkoa kwa mkoa kumuombea kura Mhe. Samia Suluhu Hassan. Ni kiongozi aliyeonyesha dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo Watanzania na hivyo anatakiwa kupewa nafasi ya kuendelea na uongozi,” amesema Chifu Sangalali.

Mbali na siasa, Chifu huyo ametumia jukwaa hilo kuhimiza wananchi kuendeleza mila na desturi za asili kwa kuwarithisha watoto wao ili waweze kukua katika misingi ya maadili mema yanayolinda jamii.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Vicent Anney, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Chifu Antonia katika maendeleo ya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.

Anney ameeleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana naye katika kuimarisha maendeleo ya kijamii, ulinzi na usalama pamoja na kuendeleza historia na urithi wa utamaduni wa eneo hilo.

“Tunampongeza Chifu Antonia  kwa mchango wake mkubwa kwa serikali na wananchi. Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega naye katika jitihada za maendeleo na kulinda mila na desturi za asili,” amesema Mkuu wa Wilaya.

Baadhi ya wananchi kutoka himaya ya Jigoku ambao wamehudhuria tamasha hilo wamepongeza hatua ya Chifu Antonia  kuendeleza tamasha la kitamaduni kila mwaka, wakisema linasaidia kuimarisha mshikamano wa kijamii. Wamesema wataendelea kumuunga mkono kiongozi wao katika jitihada zake za kuendeleza jamii na kuunga mkono maendeleo ya taifa.

Tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwemo Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, viongozi wa kimila, Mwenyekiti wa waganga wa tiba asili wilayani humo pamoja na wadau wa maendeleo.

Aidha, burudani za ngoma za asili pamoja na wasanii wa nyimbo za kitamaduni zilitumbuiza hadhira, akiwemo Nhelemi Mbasando na Ng'wana Kang'wa, ambao wamekabidhiwa tuzo za heshima kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kuenzi na kuendeleza nyimbo za asili miongoni mwa jamii ya Wasukuma.

Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.

Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Vicent Anney akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni himaya ya Jigoku 2025, ambapo amempongeza chifu Antonia Sangalali kwa kuendeleza utamaduni wa eneo hilo.






GUSA LINK HAPA CHINI👇


🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post