
Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,
amehutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika mjini Shinyanga, ambapo
ameeleza kwa kina mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi
wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwaomba wananchi kuendelea kumuunga
mkono ili kuendeleza amani na maendeleo ya taifa.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika
mkutano huo, Dkt. Nchimbi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa
kiwango kikubwa katika miradi ya maendeleo katika sekta muhimu za kijamii na
kiuchumi ikiwemo elimu, afya na miundombinu, hatua ambayo imeleta mageuzi ya
kweli yanayogusa maisha ya wananchi katika kada mbalimbali.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa
Shinyanga kumpa kura nyingi Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu ujao ili aendelee
kuongoza nchi kwa amani, mshikamano na maendeleo ya haraka zaidi.
Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa ushindi wa Rais Samia
utakuwa na maana kubwa zaidi iwapo wananchi pia watawachagua wabunge na
madiwani wa CCM, kwa kuwa kufanya hivyo kutaipa Serikali nguvu ya kutekeleza
Ilani ya Chama bila vikwazo, jambo litakaloharakisha utekelezaji wa miradi na
ahadi zilizotolewa kwa wananchi wa Shinyanga na Watanzania kwa ujumla.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini,
Mhe.Patrobas Katambi, ametumia nafasi hiyo kutoa maelezo ya kina kuhusu utekelezaji
wa Ilani ya CCM 2020–2025 katika sekta mbalimbali ndani ya jimbo hilo na mkoa
wa Shinyanga kwa ujumla.
Katambi amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia,
kumekuwa na mageuzi makubwa katika sekta za miundombinu, elimu, afya, maji safi
na salama pamoja na ajira kwa vijana, jambo ambalo limekuwa mkombozi mkubwa kwa
wananchi wa Shinyanga.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa, Itikadi, Uenezi na
Mafunzo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Bwana. Richard Raphael Maselle, amesema ziara
ya Dkt. Nchimbi itaendelea kesho Septemba 4, 2025, ambapo atahutubia wakazi wa Kata
ya Isaka, kisha ataelekea Kata ya Kagongwa wilayani Kahama na kuhitimisha kwa
mkutano mkubwa katika eneo la maegesho ya magari, Mtaa wa Majengo, Manispaa ya
Kahama.
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Rais, Wabunge na Madiwani watachaguliwa, huku CCM ikinadi Ilani yake mpya ya miaka mitano ijayo yenye dhamira ya kuijenga Tanzania yenye maendeleo, mshikamano na ustawi kwa Watanzania wote.

Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, akimuombea kura za ndiyo mgombea wa ubunge jimbo la Shinyanga mjini kupitia CCM, Paschal Patrobas Katambi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment