" DKT. LUZILA ATOA WITO KWA WANANCHI KUPIMA AFYA MARA KWA MARA BAADA YA MWITIKIO MKUBWA WA KAMBI YA NCDs

DKT. LUZILA ATOA WITO KWA WANANCHI KUPIMA AFYA MARA KWA MARA BAADA YA MWITIKIO MKUBWA WA KAMBI YA NCDs

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Luzila John, ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kutambua mapema changamoto za kiafya na kupata ushauri sahihi kutoka kwa wataalamu.

Dkt. Luzila ametoa kauli hiyo leo Novemba 15, 2025, wakati wa kuhitimisha Kambi ya Upimaji wa Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) iliyofanyika kwa muda wa siku tano katika Viwanja vya Zimamoto mjini Shinyanga.

Amesema lengo la kambi hiyo lilikuwa kuwafikia watu 500, lakini mwitikio umekuwa mkubwa zaidi baada ya wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Katika upimaji huo, watu 232 waligundulika kuwa na shinikizo la damu, 55 matatizo ya sukari, 307 uzito uliokithiri, huku 27 wakibainika kuwa na uzito pungufu.

Dkt. Luzila amesema wananchi kuanzia miaka 18 na kuendelea wanapaswa kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kuathiri maisha yao.

Ameongeza kuwa kupitia kambi hiyo pia wamefanikiwa kukusanya uniti 25 za damu salama, huku kuwasisitiza wananchi kujitokeza kuchangia damu, na akibainisha kuwa uhitaji bado ni mkubwa hasa kwa wajawazito na watoto.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima, akiwamo Emmanuel Kayange, wameishukuru Hospitali kwa kuandaa kambi hiyo iliyowawezesha kupata huduma muhimu na kujua hali zao za afya, sambamba na kuhamasishwa kubadili mtindo wa maisha.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Luzila John.


Post a Comment

Previous Post Next Post