📌 *Majiko banifu 1,583 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku*
📌 *Jiko moja kuuzwa kwa bei ya ruzuku TZS 11,200* .
📍 *HANANG*
Wakazi wa Hanang waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 19 Novemba, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mheshimiwa Almishi Hazali wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku.
"Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika kutunza na kuhifadhi mazingira" alisema Mhe. Hazali.
Mradi huu unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika kutunza mazingira na kuboresha afya za wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Aidha Serikali imeweke ruzuku ya asilimia 80 katika kila jiko ili kumpunguzia mwananchi hususani wa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji gharama ya kununua jiko na hivyo badala ya mwananchi kununua jiko kwa Tsh 56,000 atanunua kwa Tsh 11,200 pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Afisa masoko wa kampuni ya L’S Solution ambayo ndio kampuni itakayo sambaza majiko hayo, Ndugu Henry Isack amesema,"Mradi huu unakuja kubadilisha mtazamo wa wananchi katika matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kutoka kutumia kuni na mkaa mwingi mpaka kutumia kuni na mkaa kidogo wakati wa kupika".
Aliongeza kwa kusema majiko haya yametengenezwa kwa nyenzo ambazo zinasaidia jiko kuhifadhi joto kwa mda mrefu hivyo kupunguza matumizi makubwa ya mkaa na kuni
Aidha majiko haya hayatoi moshi na hivyo kupunguza uzalishaji wa sumu itokanayo na kuni na mkaa ambayo husababisha magonjwa yanayochangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba.
Aidha mheshimiwa Hazali, ameishukuru na kuipongeza REA pamoja na mtoa huduma kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa majiko banifu kwa bei nafuu na yenye ufanisi mkubwa wakati wa utumiaji.
Mwisho


Post a Comment