Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka watawa kutambua kuwa, maisha ya wakfu waliyoyachagua ni maisha ya kujitoa sadaka kikamilifu bila kujibakiza, kwa ajili ya Mungu na Kanisa lake.
Askofu Sangu amesema hayo leo Jumamosi tarehe 13.12.2025, kupitia mahubiri yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kufunga nadhiri za kwanza kwa watawa watano wa Shirika la kijimbo la Bikra Maria Mama wa Huruma, iliyofanyika leo katika Kanisa Kuu la Mama wa Huruma Ngokolo, mjini Shinyanga.
Askofu Sangu amewasisitiza watawa hao kuziishi kwa uaminifu nadhiri walizoapa mbele ya Mungu na Kanisa za utii, usafi kamili na ufukara, kwa kuzingatia amri za Mungu pamoja na mafundisho ya Yesu Kristo.
Ameelezea kuwa, nadhiri ya utii ni msingi muhimu wa maisha ya wakfu na kwamba, hiyo ndiyo inamwezesha mtawa kuziishi kikamilifu nadhiri nyingine.
Amewatahadharisha watawa kuepuka kiburi, akibainisha kuwa ni kinyume cha utii na hakiwezi kuleta mafanikio katika utume wao.
Aidha, Askofu Sangu amewaomba waamini kuendelea kusali kuwaombea watawa hao ili waweze kuyaishi kwa uaminifu maisha ya sadaka waliyochagua, pamoja na kuombea uthabiti wa familia ambazo ndiyo chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa.
Watawa waliofunga nadhiri zao za kwanza katika Shirika la Kijimbo la Bikra Maria Mama wa Huruma ni pamoja na Sister Clesencia Shirima kutoka Jimbo Katoliki Moshi, Sister Restuta Remiji kutoka Jimbo la Mbulu, Sister Jackrine Joseph Mwandu kutoka Parokia ya Maganzo, Jimbo la Shinyanga, Sister Eunice Thomas kutoka Jimbo la Geita pamoja na Sister Sarah Masanja kutoka Parokia ya Maganzo, Jimbo la Shinyanga.
Watawa hao wamefunga nadhiri zao mbele ya Askofu Liberatus Sangu pamoja na Mlezi mkuu wa Shirika, Sister Christina Mwansanga, ambaye ni Mama Mkuu wa Shirika la Maria Malkia wa Mitume kutoka Jimbo la Mbeya.
Post a Comment