
Rais wa Klabu ya Young Africans SC (Yanga) na Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu Afrika (ACA), Eng. Hersi Said, ameweka wazi msimamo wake kufuatia mjadala ulioibuka mitandaoni unaohusisha klabu ya Simba SC, akisisitiza kuwa hakuwahi kudharau wala kudai kuwa Simba haina uongozi mzuri.
Akizungumza katika mahojiano yaliyonukuliwa na SportsXtra, Eng. Hersi amesema kuwa lengo la wasilisho (presentation) alilofanya halikuwa kuishambulia Simba bali lililenga kuzungumzia kwa mapana maendeleo ya vilabu barani Afrika na mabadiliko yanayohitajika katika mifumo ya uendeshaji wa vilabu hivyo.
“Kwanza nikupongeze kwa kutafuta taarifa sahihi. Kuna watu badala ya kutafuta ukweli wamejikita katika mdahalo usio sahihi kwamba kulikuwa na masimango yamefanywa kwa Klabu ya Simba, jambo ambalo sio kweli kabisa,” amesema Eng. Hersi.
Ameeleza kuwa katika wasilisho lake kulikuwa na maeneo matatu makuu aliyoyazungumzia, mojawapo likiwa ni changamoto zinazovikabili vilabu vya Afrika kwa ujumla. Katika eneo hilo, alitumia mfano wa mashabiki wa Simba kama sehemu ya ufafanuzi wa changamoto, lakini si kwa lengo la kuonyesha kuwa klabu hiyo haina uongozi mzuri.
“Eneo la kwanza nilizungumzia changamoto za vilabu vya Afrika. Ukizungumzia changamoto hizo, hakuna mahali nilipotamka au kuashiria kwamba Simba haina uongozi bora. Mfano uliotumika ni wa mashabiki wa Simba, lakini haukuwa na tafsiri wala maana ya kudhalilisha uongozi wa klabu hiyo,” alifafanua.
Eng. Hersi pia ametumia fursa hiyo kutoa heshima kwa viongozi wa Simba SC akiwataja Mwenyekiti Mangungu na Afisa Mtendaji Mkuu, Magori, kama viongozi wenye uwezo na uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Namuheshimu sana Mangungu, namuheshimu sana kaka yangu Magori. Wote hawa ni viongozi wazuri na wana uzoefu mkubwa kwenye mpira. Tunachokizungumza hapa ni dhana ya utawala bora (good governance) na siyo uongozi bora (good leadership),” alisisitiza.
Kauli ya Eng. Hersi imekuja wakati ambao mashabiki wa soka nchini wanaendelea kufuatilia kwa karibu mijadala kuhusu uendeshaji wa vilabu vikubwa, hasa Simba na Yanga, ambazo zimekuwa nguzo muhimu za maendeleo ya soka la Tanzania.
Kwa ujumla, Eng. Hersi amewataka wadau wa soka na mashabiki kujifunza kutenganisha hoja za kitaalamu kuhusu mifumo ya utawala wa vilabu na masuala ya kihisia yanayoweza kuchochea migogoro isiyo na msingi, akisisitiza kuwa maendeleo ya soka la Afrika yanahitaji mjadala wa kina, hoja zenye msingi na mshikamano baina ya vilabu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment