" MBUNGE MUTASINGWA ASHEREKEA CHRISTMAS NA WATOTO YATIMA,AWAHIMIZA WANANCHI KUUNGANA KUWASAIDIA WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU.

MBUNGE MUTASINGWA ASHEREKEA CHRISTMAS NA WATOTO YATIMA,AWAHIMIZA WANANCHI KUUNGANA KUWASAIDIA WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU.


‎Na Fabius Clavery,Misalaba Media-Kagera.‎Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera, Mhandisi Johnston Mutasingwa, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kuendelea kujitokeza kwa moyo wa kujitolea kusaidia mahitaji mbalimbali katika vituo vya kulelea watoto wanaotoka katika mazingira magumu, ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.‎Mhandisi Mutasingwa ametoa wito huo, baada ya kutembelea vituo vitatu vinavyolea watoto wanaotoka katika mazingira magumu ndani ya Jimbo la Bukoba Mjini, wakati akisherekea na kutoa  zawadi za sikukuu ya Krismasi 2025 na Mwaka Mpya 2026 kwa watoto waliopo katika vituo hivyo.‎Katika ziara hiyo, mbunge huyo amekabidhi zawadi mbalimbali zikiwemo mchele, mboga, vinywaji pamoja na vifaa vya shule kama kalamu na madaftari, kwa lengo la kuwafariji watoto hao na kuunga mkono juhudi za vituo vinavyowalea.‎Vituo vilivyotembelewa ni pamoja na Tumaini Children Centre, Uyacho Turkey Orphanage Centre, pamoja naKituo cha Kulelea Watoto cha Nusuru Yatima Bukoba.‎Akizungumza katika Kituo cha Nusuru Yatima Kashai, Mhandisi Mutasingwa amesema atarejea tena tarehe 28 Desemba ili kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la watoto, huku akiahidi kuwa mradi huo utatekelezwa ndani ya mwaka mmoja.‎“Nitarudi hapa tarehe 28, tutatembelea eneo lililopo tuone namna bora ya kujenga bweni la watoto wetu hapa Nusuru, na tutalifanya hilo ndani ya mwaka mmoja. Lakini nitoe wito kwa ndugu zangu Wanabukoba Mjini, tujitolee kile tulichonacho kwa ajili ya watoto wetu hawa,” amesema Mhandisi Mutasingwa.‎Awali, Meneja wa Kituo cha Nusuru Yatima Bukoba, Ramadhan Rashid, kwa kushirikiana na mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Anaweza Festo, walimshukuru Mbunge Mutasingwa kwa msaada wa sikukuu za Krismasi na kueleza kuwa kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa bweni la watoto.‎Kwa upande wake, Sister Adventina Kyamanywa, msimamizi wa Tumaini Children Centre kilichopo Kata ya Nyanga, Manispaa ya Bukoba, amewaomba wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kusaidia vituo hivyo, akisema bado wapo watoto wengi wanaoishi katika mazingira hatarishi mitaani na watoto yatima ambao huhifadhiwa na kulelewa katika vituo hivyo.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post