Tanzania leo, Desemba 9, inaadhimisha miaka 64 ya
Uhuru, siku muhimu inayokumbusha safari ndefu ya kujenga Taifa lenye amani,
umoja na maendeleo.
Katika kuadhimisha siku hii, Tanzania Bloggers Network
(TBN) imetoa salamu maalum kwa Watanzania wote, ikisisitiza umuhimu wa
kutafakari tulikotoka, mahali tulipo na mwelekeo wa taifa kuelekea mbele.
Katika salamu hizo, TBN imewakumbusha Watanzania
msingi wa fikra za waasisi wa Taifa, akiwamo Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, ambaye alisisitiza kwamba uhuru kamili hauwezi kupatikana
bila kujitegemea.
Mwalimu aliwahi kusema:
“Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama
tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi.”
Amani na Mshikamano: Nguzo za Maendeleo
TBN imesisitiza kuwa maendeleo ya Taifa yamejengwa juu
ya msingi wa amani na umoja, na kwamba vurugu na uchochezi havina nafasi katika
Taifa linalotaka kusonga mbele. Ikimnukuu Rais mstaafu Benjamin William Mkapa,
TBN imesema:
“Amani si kitu cha asili, tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila
amani, hakuna maendeleo ya kweli.”
Mtandao huo umeonya kuwa kuruhusu migawanyiko na
uchochezi kunaweza kudhoofisha juhudi za kupambana na maadui watatu wa taifa—ujinga,
umaskini na maradhi—kama ilivyopangwa na waasisi wa uhuru.
Kuunga Mkono Mageuzi ya Taifa
TBN imekumbusha pia kauli ya Rais mstaafu Ali Hassan
Mwinyi:
“Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa
Taifa hili.”
Kwa sasa, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Taifa linapitia mageuzi kupitia falsafa ya 4R—Reconciliation,
Resilience, Reforms na Rebuilding. TBN imetoa wito kwa Watanzania
kuunga mkono juhudi hizi zinazolenga kuimarisha misingi ya maridhiano, mageuzi
na ustawi wa pamoja.
Tanzania Kwanza, Kazi na Utu
Katika hitimisho, TBN imewataka Watanzania kutumia
uhuru wa maoni na majukwaa ya mijadala katika kujenga Taifa, si kulivuruga.
Mtandao huo umetoa wito wa kufanya kazi kwa bidii, kudumisha amani na kuepuka
kutumika katika mipango inayolenga kuliharibu Taifa.
“Tukumbuke: Huu ni wakati wa kuzungumza kujenga, si
kubomoa,” imesisitiza TBN.
TBN imewatakia Watanzania wote Maadhimisho Mema ya
Miaka 64 ya Uhuru, ikisisitiza kauli mbiu yake:
“Tanzania Kwanza, Kazi na Utu – Tusonge Mbele.”
Imetolewa na:
Beda Msimbe
Mwenyekiti, Tanzania Bloggers Network (TBN)
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment