" ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI

ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI



Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Rashidi Mahenge na Said Suleimani wote wakazi wa Mji Mdogo wa Tunduma Mkoani Songwe kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa bila kibali.

Watuhumiwa walikamatwa huko katika kizuizi cha Polisi kilichopo eneo la Mwakapangala, Kata ya Nsalala, Mji Mdogo wa Mbalizi katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma wakiwa na wameingiza nchini bidhaa vipodozi vyenye viambata sumu vya aina mbalimbali vilivyopigwa marufuku nchini boksi 22 pamoja nyavu vya kuvulia Samaki zilizopigwa marufuku na mamlaka husika.

Aidha, watuhumiwa walikamatwa wakiwa na vitenge jola 42 bila kibali cha kuingiza bidhaa hizo nchini ambazo walizitoa nchini Zambia wakitumia gari lenye namba za usajili T371 DSS aina ya Toyota Mark X mali ya mtuhumiwa Rashidi Mahenge.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Furaha George maarufu Mwakatundu, mkazi wa Ipyana Wilayani Kyela Mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa bila kibali.

Mtuhumiwa alikamatwa huko maeneo ya Njiapanda ya Kikusya, Kata ya Itope, Tarafa ya Unyakyusa, Wilayani Kyela akiwa ameingiza nchini bidhaa Mayai ya Kuku wa Kisasa Trei 48 na Sukari Kilogramu 40 bila kibali kutoka nchini Malawi akitumia vivuko visivyo rasmi.

ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Norasco Herman Mgaya, mkazi wa Matembwe Mkoani Njombe kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno ya Tembo mawili.

Mtuhumiwa alikamatwa eneo la Mafiati Jijini Mbeya akiwa na meno mawili ya Tembo yenye uzito wa Kilogramu 1.6 akiwa ameyafunga kwenye mfuko wa Sandarusi na kuyaficha ndani ya begi dogo la mgongoni.

Mtuhumiwa alitokea Mkoani Njombe kwa basi la abiria la kampuni ya Mwendamseke akiwa na meno hayo ya Tembo kwa lengo la kutafuta wateja na kabla ya kufanikisha hadhima yake alikamatwa na Jeshi la Polisi.

Aidha, katika kuzuia na kudhibiti makosa ya usalama barabarani kwa kipindi cha kuanzia Disemba 28 hadi 31, 2025 jumla ya makosa ya usalama barabarani yalikamatwa yalikuwa 1753 sawa na shilingi 49,810,000/=, Magari yaliyokamatwa kwa madeni yalikuwa 425 sawa na shilingi 25,015,608 wakati madereva 126 walikamatwa kwa mwendo kasi na madereva 03 walikamatwa wakiendesha gari wakiwa na kiwango kikubwa cha ulevi.

Upelelezi unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tamaa ya mali kuacha kujihusisha na biashara haramu na magendo na badala yake wafuate taratibu za biashara ili kuepuka mkono wa serikali.

Aidha, Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuendelea kulinda na kutunza rasilimali za nchi na kuachana na biashara haramu za meno ya Tembo kwani wanapelekea Taifa kupoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na uwindaji haramu wanaoufanya na kukwamisha jitihada za serikali za kuingiza fedha za kigeni kutokana na Watalii kuja kuona Wanyama.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post