" DIRA YA RAIS SAMIA ILIVYOWEZESHA MAFANIKIO UKUSANYAJI KODI

DIRA YA RAIS SAMIA ILIVYOWEZESHA MAFANIKIO UKUSANYAJI KODI


Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Misalaba Media -Tanga

Tangu aingie madarakani mwezi Machi, 2021, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameonyesha dhamira ya dhati ya kuchochea ukuaji wa maendeleo nchini. Kutokana na dira yake kuchochea maendeleo, akaja na mkakati wa kukusanya kodi kikamilifu ili fedha zitakazopatikana kupitia ulipaji kodi ziweze kutumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo itakayokuwa nyenzo ya kuboresha hali za maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa letu.

Rais Dk. Samia akaweka wazi dhamira yake ya kuongeza makusanyo ya kodi bila dhulma wala matumizi ya mabavu kutoka kwa wananchi. Dk. Samia akasisitiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuepuka kufunga biashara kwa mfanyabiashara anayedaiwa kodi badala yake mazungumzo yafanyike ili mfanyabiashara anayedaiwa aendelee kufanya biashara huku akilipa deni taratibu na kuchangia maendeleo ya nchi yake.

Mwamko wa kulipa kodi umeongezeka maradufu miongoni mwa walipakodi chini kutokana na mazingira mazuri na wezeshi ya ulipaji kodi yaliyopo kwa sasa. Kutokana na hali hii, Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, TRA wamekuwa wakiongeza ukusanyaji wa kodi kila mwezi, hali inayotoa uhakika wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, maji, barabara, umeme, kilimo, masoko, uvivu, ufugaji, kutaja kwa uchache.

Kwa mfano,  kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alipokuwa akiongea na vyombo vya habari Januari 1, 2026, alisisitiza kuwa kwa mwezi Desemba, 2025, TRA wamefanikiwa kukusanya kodi kiasi cha Shilingi Trilioni 4.13 sawa na asilimia 102.9 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 4.01. Rekodi hii ni ya kipekee tangu kuanzishwa kwa TRA. "Mhe. Rais amejenga uhimilivu wa shughuli za uchumi ambao umeonyesha matokeo katika makusanyo ya kodi na miongozo ambayo tumekuwa tukipewa na Serikali ya Awamu ya Sita imeonyesha kuwa na matunda" amesema Mwenda.

Aidha, katika kusisitiza mageuzi na mapinduzi makubwa ya ukusanyaji kodi nchini, Kamishna Mwenda amesema katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025, Mamlaka imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 9.8 sawa ma asilimia 101.45 ya lengo la kukusanya Trilioni 9.66. Kwahiyo, mikakati madhubuti iliyoratibiwa, imewezesha mafanikio katika ukusanyaji wa kodi na hivyo kutoa uhakika wa kukamilika kwa miradi ya maendeleo ambayo wananchi wanaisubiria kwa hamu kubwa.

Kwa hakika, kazi kubwa imefanyika kuhakikisha makusanyo ya kodi yanaongezeka. Wananchi kwa upande wao wamehamasika kulipa kodi kwani wameona namna kodi wanazolipa zinavyotumika vizuri katika miradi ya maendeleo yenye tija kwa maisha yao na nchi yao pia. Nihitimishe Makala hii kwa kusema: Kama Taifa, tunapaswa kuwa kitu kimoja, tulipe kodi kwa hiari bila shuruti ili Taifa letu liweze kujitegemea kiuchumi kwa kutumia fedha zetu wenyewe kugharamia miradi ya maendeleo, hili litatujengea heshima kitaifa na kimataifa..

 

Post a Comment

Previous Post Next Post