Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wamepewa wito wa kuhakikisha wanaanza kulima na kufuga kwa tija ili kuinua uchumi wao na wa mkoa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Karagwe Development and Relief Services (KADERES), Leonard Kachebonaho, wakati akizungumza na redio Kasibante FM jana tarehe 02 Januari 2026.
Kachebonaho amesema Mkoa wa Kagera una bahati kubwa ya kuwa na mvua mara mbili kwa mwaka pamoja na vyanzo vya maji vya kutosha ikiwemo Ziwa Victoria na Mto Kagera, hali inayowezesha mazingira mazuri ya kilimo na ufugaji wenye tija.
Aidha, amewataka vijana kuacha kufanya shughuli zao mmoja mmoja na badala yake kuungana katika vikundi au ushirika, akisisitiza kuwa kufanya kazi kwa pamoja kunarahisisha upatikanaji wa mitaji, mikopo na fursa mbalimbali kutoka sekta binafsi, mashirika na serikali.
“Mimi nawasihi vijana waungane na wawe na malengo ya pamoja, maana ni rahisi kufikika kwa namna mbalimbali. Serikali imeunda Wizara ya Vijana na imeweka fursa nyingi sana. Vijana wakikaa wamebweteka, umasikini utawafuata popote, lakini fursa zinatafutwa,” amesema Kachebonaho.
Ameongeza kuwa hata vijana wanaotoka katika familia maskini wana nafasi kubwa ya kubadilisha maisha yao endapo wataamua kuchangamkia fursa zilizopo na kufanya kazi kwa bidii na mshikamano.
Vilevile, Kachebonaho amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa, kwa jitihada zake za kuhamasisha uwekezaji na kuandaa fursa mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wananchi wa Kagera kuinuka kiuchumi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment