Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma umezidi kuchukua sura mpya ambapo kwa sasa utekelezaji wake umefikia hatua kubwa ya asilimia 94 katika miundombinu na asilimia 65 kwa upande wa majengo.
Hatua hii ni kielelezo tosha cha safari ya Tanzania kutoka katika ramani na michoro ya kinadharia kuelekea katika uhalisia wa kimkakati ambao unakwenda kuibadilisha Dodoma kuwa kitovu cha usafiri wa anga barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Kukamilika kwa uwanja huu si tu faraja kwa wasafiri, bali ni ufunguzi wa mnyororo mpana wa fursa za kiuchumi ambao unahitaji maandalizi ya dhati kwa nguvukazi ya ndani, hususan vijana, ili waweze kushiriki kikamilifu katika soko la ajira lenye ushindani mkubwa.
Katika kuhakikisha kuwa uwanja huu unakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati ya makusudi ya kukuza ujuzi kwa vijana kupitia programu za uanagenzi na mafunzo ya ufundi stadi. Hatua hii inalenga kuandaa vijana hodari watakaoweza kuhudumia mnyororo wa thamani wa uwanja huu mkubwa, kuanzia katika ufundi wa mitambo, uhandisi wa majengo, huduma za anga, na teknolojia ya kisasa ya usalama.
Ni wazi kuwa uwanja wenye hadhi ya kimataifa kama wa Msalato unahitaji utaalamu wa hali ya juu na nidhamu ya kazi, hivyo programu hizi za uanagenzi ndizo zinazowajengea vijana msingi wa kuwa wachapakazi hodari wanaoweza kushindana si tu hapa nchini, bali hata katika soko la ajira la kimataifa.
Uwepo wa uwanja huu unakwenda kufungua milango ya ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, huduma za ukarimu, na biashara ya usafirishaji wa bidhaa za kilimo zinazohitaji kufika sokoni kwa haraka.
Kupitia maandalizi ya kijana mmoja mmoja katika kupata ujuzi wa vitendo, Tanzania inatengeneza jamii inayoweza kujiajiri na kuajiri wengine katika maeneo yanayozunguka mradi huu. Hii ni fursa kwa vijana kuelewa kuwa kuwa na uwanja mkubwa duniani ni jambo moja, lakini kuwa na wataalamu wazawa wenye uwezo wa kuuendesha na kuufanya uwe na tija ni jambo lingine muhimu zaidi ambalo Serikali inalipa kipaumbele kwa sasa.
Msalato sasa inatazamwa kama lango kuu la biashara linalounganisha Tanzania na nchi nane jirani pamoja na masoko ya Mashariki ya Kati na Mbali, jambo linalohitaji utayari wa hali ya juu wa nguvukazi ya ndani. Kutoka kuwa ndoto iliyoandikwa kwenye karatasi hadi kuwa ukweli unaoonekana kwa macho, mradi huu unawakumbusha Watanzania wajibu wa kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo huku wakijiandaa kuitumia kama jukwaa la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment