Na Lydia Lugakila -Misalaba MediaMbeyaUmoja wa Ujirani Mwema Ilomba Block D, mkoani Mbeya, umetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja katika Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Bi Aisha Foundation, kilichopo Kata ya Ruanda, Mtaa wa Soweto.Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwaunga mkono watoto yatima katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.Akizungumza na Misalaba Media mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Ujirani Mwema Ilomba Block D, Bi. Neema Mwangwala, amesema umoja huo wa akina mama umejiwekea utaratibu wa kutembelea na kusaidia wenye uhitaji kila mwaka.Ameeleza kuwa kabla ya kufikisha msaada huo, walifanya tathmini na kubaini kuwa kituo cha Bi Aisha Foundation kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowaathiri watoto wanaolelewa hapo.“Leo tumetoa hiki kidogo kilichotokana na michango yetu binafsi tunaamini tutafikia malengo tuliyojiwekea, ikiwemo kuongeza utoaji wa misaada angalau mara mbili au hata nne kwa mwaka,” alisema Bi. Mwangwala.Aidha, mwenyekiti huyo amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa umoja huo, wamefanikiwa kufika katika maeneo mbalimbali yenye wahitaji ambapo miongoni mwa maeneo hayo ni Gereza la Ruanda, walikokwenda kuwafariji wanawake wafungwa, pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, walikotoa msaada kwa watoto waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la utapiamlo.Bi. Mwangwala ameongeza kuwa, pamoja na kutoa misaada, wanachama wa umoja huo wamekuwa wakishiriki pia shughuli za kijamii kama njia ya kuimarisha mshikamano, wakiamini kuwa maisha ni kushirikiana katika shida na raha.Kwa upande wake, Bi. Aisha Rajab kutoka kituoni hapo aliwashukuru wanawake hao kwa msaada walioutoa, akieleza kuwa kulikuwa na uhitaji mkubwa wa baadhi ya mahitaji yaliyowasilishwa.“Mmetujia kama mmetumwa na Mwenyezi Mungu, kwani mahitaji haya yalikuwa muhimu sana kwa watoto wetu,” alisema Bi. Aisha.Bi Rajabu ameeleza kuwa kituo hicho kinahudumia watoto yatima wa dini zote makabila yote wa kuanzia umri wa miaka 0 hadi 18.Aidha, amewahamasisha wadau na jamii kwa ujumla kuendelea kufanya matendo ya huruma kama yalivyofanywa na Umoja wa ujirani Mwema.Ameongeza kuwa kwa sasa kituo hicho kina jumla ya watoto 24 wa kike na wa kiume. Pia kinatarajia kuanza ujenzi wa miundombinu mipya pindi kitakapopata kibali kutoka kwa mamlaka husika, kwa kuwa eneo walilonalo ni dogo na halitoshelezi mahitaji ya watoto hao.Naye Afisa Habari wa Umoja wa Ujirani Mwema, Ester Kinyaga, amewapongeza wanachama wa umoja huo kwa kuendeleza desturi ya kuwajali na kuwafariji wenye uhitaji.Bi. Kinyaga amesema kuwa kutoa msaada ni aina ya sadaka mbele za Mungu na kwamba hali ya uyatima inaweza kumkumba mtu yeyote bila kutarajia.Hata hivyo, amewahimiza wanawake wa makundi mengine pamoja na watu binafsi kujitokeza kutembelea na kusaidia wenye uhitaji, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni njia ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kupata baraka kutoka kwa mwenyezi Mungu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment