
NA DENIS MLOWE, IRINGA
MABANDA ya wafanyabiashara wadogo katika eneo la Garden, linalomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, yameteketea vibaya baada ya moto mkubwa kuzuka usiku wa saa tano.
Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku mamlaka husika zikiendelea na uchunguzi.Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amesema moto huo ulikuwa mkali na umeharibu mabanda karibu yote yaliyokuwa katika eneo hilo upande wa boma ambalo ni maarufu kwa shughuli za biashara ndogo na vivutio vya utalii.
“Moto umeunguza mabanda mengi pamoja na bidhaa zote zilizokuwamo ndani hili ni eneo la utalii, na wafanyabiashara wengi hapa ni wajasiriamali wadogo waliokuwa wakitegemea mikopo, ikiwemo ya wanawake na vijana. Hasara ni kubwa sana,” amesema.Amesema kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilifika eneo la tukio na kufanya juhudi kubwa kudhibiti moto huo, ingawa sehemu kubwa ya mabanda ilikuwa tayari imeshateketea.
“Hadi sasa tunafanya tathmini kujua kiasi cha hasara na idadi kamili ya waliopatwa na madhara ya mali. Tunamshukuru Mungu kwani hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha,” amesema Sitta.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wote waliopata hasara kujitokeza ili kuandikishwa kwa ajili ya tathmini rasmi, huku akiahidi kuwa taarifa zaidi zitatolewa pindi uchunguzi utakapokamilika.
Baadhi ya wafanyabiashara waliounguiwa na vibanda hivyo wakizungumza kutokana janga hilo wanasema moto ulianza majira ya saa 5 kasoro, ambapo walinzi wa soko wanasemekana kuwa wa kwanza kuona cheche za moto nyuma ya moja ya vibanda kabla haujasambaa kwa kasi.
Biashara nyingi zilizoteketea zilihusisha bidhaa zinazowaka haraka kama nguo, masponchi, miti ya kutundikia bidhaa na vifaa vingine vilivyokuwa ndani ya vibanda hivyo, hali iliyoufanya moto kuenea kwa haraka.
Rescue Kebodia, mmoja wa wafanyabiashara walioathirika, alisema kuwa juhudi za awali za kuokoa mali hazikufanikiwa kutokana na ukubwa wa moto.
“Moto ulikuwa mkubwa sana. Tulijitahidi lakini hatukuweza kuokoa chochote. Kikosi cha zimamoto kilifika na kuanza kupambana, lakini tayari moto ulikuwa umeenea,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Iringa Masai Market, Musa Julius alisema kuwa hatua za haraka zilichukuliwa mara tu taarifa zilipopokelewa, ikiwemo kutoa taarifa kwa kikosi cha zimamoto kilichopo karibu na eneo hilo.
“Nilifika mapema na kuwataarifu zimamoto. Walijitahidi kupambana lakini moto ulikuwa umeshika nguvu kutokana na aina ya bidhaa zilizokuwapo ndani. Karibu vibanda 20 vimeathirika,” alisema
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amesema kuwa tathmini kamili ya hasara bado haijafanyika kutokana na ugumu wa kukusanya taarifa za wafanyabiashara wote usiku wa tukio.
“Tunasubiri wafanyabiashara wote wakusanyike leo ili kila mmoja awasilishe taarifa ya mali na hasara zake kwani vigumu kwa sasa kusema hasara ni kiasi gani, lakini athari ni kubwa sana,” aliongeza.
Aidha, ilibainika kuwa wafanyabiashara walio wengi hawana bima ya biashara, jambo linaloongeza ukubwa wa athari kwao mara baada ya tukio hilo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment