Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, ameeleza mafanikio, malengo na mwelekeo wa operesheni maalum ya Vijana Daka Fursa na Samia iliyotekelezwa katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Kagera kuanzia Februari 20 hadi 27,2026.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 28 2026,Buruhani amesema operesheni hiyo imelenga kuhamasisha vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Amesema katika ziara hiyo walikutana na vijana katika halmashauri zote nane na kutoa elimu kuhusu namna ya kuunda vikundi, kuandaa maandiko ya miradi na kufuata taratibu sahihi za kupata mikopo hiyo. Aidha, UVCCM imehimiza uwazi na usimamizi mzuri wa mikopo ili kuhakikisha inawanufaisha walengwa na kurejeshwa kwa wakati.
Kwa mujibu wa Buruhani, operesheni hiyo imeongeza mwamko kwa vijana wengi kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali, hususan katika sekta za kilimo, uvuvi, biashara ndogo na huduma mbalimbali.
Ameongeza kuwa Zaidi ya vikundi 59 vya vijana mkoani Kagera vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kutoka halmashauri zote ikiwa asilimia nne ni maalumu kwa ajili ya kundi la Vijana. Vikundi hivyo vimepata shilingi bilioni 1,383,111,000 kwa ajili ya kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi katika mwaka wa Fedha 2024/2025 na 2025/2026.
Amesema fedha hizo zimechangia kuongeza ajira kwa vijana pamoja na kuwawezesha wengi kujiajiri katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda vidogo. Kupitia mitaji hiyo, vijana wengi wamefanikiwa kuboresha kipato na kuinua hali zao za maisha.
Aidha, ametoa shukrani kwa serikali kwa kuendelea kutenga fedha za kuwawezesha vijana kupitia mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na fedha zinazotolewa na serikali zinazofikia zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.



Post a Comment