" TAKUKURU SHINYANGA YALETA MAPINDUZI SEKTA YA AFYA USHETU, MAADILI, UWAJIBIKAJI WAIMARIKA NA MAPATO YAPAA KUTOKA MILIONI 3 HADI 13.

TAKUKURU SHINYANGA YALETA MAPINDUZI SEKTA YA AFYA USHETU, MAADILI, UWAJIBIKAJI WAIMARIKA NA MAPATO YAPAA KUTOKA MILIONI 3 HADI 13.

Na Moshi Ndugulile

Mapato ya Idara ya Afya katika Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama, yameongezeka kutoka shilingi milioni 3 hadi shilingi milioni 13 kwa mwezi, sawa na ongezeko la asilimia 366. Ongezeko hilo linatajwa kuwa matokeo ya maboresho ya kiutendaji yaliyotokana na mafunzo ya maadili, uwajibikaji na madhara ya rushwa yaliyotolewa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga.

Katika  taarifa yake ya  utendaji wa taasisi hiyo, kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, aliyoitoa kwa vyombo vya habari  leo Februari 04,2026 Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Donacian Kessy, amesema mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa afya katika Halmashauri ya Ushetu na kulenga kuimarisha uadilifu pamoja na kuongeza uwajibikaji kazini.

 Kupitia elimu hiyo, watumishi wamejengewa uelewa mpana kuhusu athari za rushwa na umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga amesema  kabla ya maboresho hayo kulikuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi, ikiwemo upotevu wa mapato na huduma zisizoridhisha katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Hata hivyo, baada ya utekelezaji wa mafunzo hayo, hali imebadilika na kuleta matokeo chanya yanayoonekana.

Bwana Kessy amesema kuimarika kwa uadilifu miongoni mwa watumishi kumeongeza ufanisi katika utendaji kazi wa sekta ya afya, hali iliyochangia kukusanywa kwa mapato kwa uwazi na ufanisi zaidi,kwani  ongezeko hilo la mapato limewezesha kuboreshwa kwa huduma katika vituo vya afya, ikiwemo upatikanaji wa huduma kwa wakati na kwa haki kwa wananchi wote.

Aidha, maboresho hayo yameongeza imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na sekta ya afya katika halmashauri hiyo, ikilinganishwa na awali, ambapo kulikuwa na malalamiko ya mara kwa mara, lakini kwa sasa wananchi wanashuhudia mabadiliko chanya yanayotokana na usimamizi madhubuti na uwajibikaji ulioboreshwa.

Kwa ujumla, hatua ya kutoa mafunzo ya maadili na kupambana na rushwa imeonekana kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya afya ya Halmashauri ya Ushetu, yakionesha kuwa uwajibikaji na uadilifu vina mchango mkubwa katika kuongeza mapato na kuboresha huduma kwa jamii.

MWISHO

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post