Na Mwandishi wetu - Kahama. Baadhi ya vijana wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kuyarejesha katika hali ya kawaida majengo yaliyokuwa yakitoa huduma kwa wananchi, ambayo yaliharibiwa katika ghasia za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa oktoba 2025.Wamesema wako tayari kushirikiana na serikali kurejesha miundombinu hiyo ili waendelee kupata huduma kama awali kutokana na hali ya upatikanaji wa huduma za serikali za mitaa na kata kupatikana kwa kusuasua huku wengine wasijue wapi ofisi zilipo.Wamefikisha ombi lao mbele ya mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda, kwenye mkutano uliolenga kueleza changamoto za upatikanaji wa huduma za wenyeviti na watendaji, ambao ofisi zao zilichomwa moto katika ghasia hizo, hali iliyosababisha kushindwa kuendelea kutumika kwa majengo hayo.Vijana hao, wakiwemo waendesha bodaboda, waendesha bajaji, wananchi wa kawaida na mafundi ujenzi, kabla ya kutoa msimamo wao, wametembelea na kukagua miundombinu iliyoharibiwa zikiwemo ofisi za kata, mitaa na vituo vya polisi.Mwenyekiti wa chama cha mafundi ujenzi Kahama (CHAMAUKA) Baraka Majengo, amesema mafundi ujenzi Kahama wako tayari kushiriki shughuli ya ukarabati wa majengo hayo kwa gharama ndogo ili waendelee kupata huduma."Tunahangaika mno sasa hivi kupata huduma, sisi tuko tayari kushirikiana na serikali kukarabati hizi ofisi kwa kujitolea kwa gharama ndogo, nimehangaika mno nikifuatilia nyaraka nipate kibali cha ujenzi, ofisi haipo, hata sijui ilipohamishiwa, ni shida sana."Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Pikipiki za Biashara Mkoa wa Shinyanga Idisam Mapande, amesema kukosekana kwa ofisi za kata kwenye maeneo yao kumeathiri ukuaji wa biashara hiyo kwa vijana, kutokana na kuchelewa kupatikana kwa baadhi ya nyaraka kutoka kwa watendaji kata.Amesema wapo vijana walijitokeza kuomba mikopo ya Halmashauri, lakini kutokana na kukosekana kwa huduma za wenyeviti na watendaji kwa wakati, wameshindwa kupata mikopo hiyo huku shughuli za biashara zikiendelea kuwa ngumu kwao.Amesema kwa kushirikiana na maafisa usafirishaji wilayani Kahama, wako tayari kuchangia mifuko kadhaa ya saruji wakati serikali itakapoanza ukarabati wa majengo hayo.Amesema " Sisi maafisa usafirishaji tumeahidiwa mikopo ya Halmashauri, lakini ili kuipata ni lazima uanzie serikali za mitaa, baadhi ya maeneo ofisi ziliharibiwa, hili limetuchelewesha kwa sababu wengi hatujui hizi ofisi zilihamia wapi, vijana wanakosa matumaini ya kuendelea na biashara hii."Asha Maulid ni mkazi wa Shunu, Kahama, amesema hali ya upatikanaji wa huduma kutoka kwa wenyeviti wa mitaa na watendaji imekuwa ngumu tofauti na ilivyokuwa awali, kwani wanalazimika kutembea umbali mrefu kupata huduma, huku gharama pia zikiongezeka.Amesema "Upatikanaji wa huduma ni mgumu kwa sasa, tunatumia muda mrefu na gharama kuwafuata walipo, lakini ni kwa sababu tuliziharibu wenyewe, serikali ituhurumie izikarabati na sisi tutahakikisha tunalikamilisha hili, akina mama tutasogeza hata maji kwa mafundi ilimradi tukamilishe."Edward Ibrahim Mkazi wa Mhongolo Kahama amesema wanapohitaji huduma ya mhuri haipatikani kwa wakati huku utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu zikiishia mtaani kutokana na kukosekana kwa kituo kidogo cha polisi na ofisi za karibu za viongozi wa serikali za mtaa.Amesema "Unahitaji huduma ya kugongewa mhuri, uanze kumtafuta mwenyekiti, mara unamkuta pembeni ya gati la maji pale, wakina mama wakiwa na kesi wengine uwezo mdogo wanashindwa kufika kituo kikubwa cha polisi, hiki kilishachomwa, wanabaki wameonewa, wanakosa haki zao." Kambai Manyenye ni Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mhungula, Kahama, ameomba mamlaka kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kurejesha majengo hayo ili huduma ziendelee kutolewa kwani wananchi wengi wanahangaika kuzipata.Ameishukuru serikali katika baadhi ya maeneo kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa wananchi licha ya changamoto zilizopo za umbali huku kukikosekana bajeti rasmi ya kuwafikisha ofisini na kurejea nyumbani."Tunajibanza pembeni ya ofisi nyingine kutoa huduma kwa wananchi wetu, kila kitu kilichomwa moto hatuna hata meza, unaandika umesimama, unagonga mhuri umesimama, ukitoka hapo umechoka mno, kwa kweli hizi ofisi ziangaliwe na sisi tuko tayari kuunga mkono shughuli ya ujenzi tuondokane na hii changamoto."Diwani wa kata ya Kahama Mjini Andrew Godson amesema "Kitendo hiki kinaonyesha maridhiano baina yetu sisi wawakilishi wa wananchi na hawa vijana, hii tunasema ni historia, tupo tayari kuungana nao, huduma katika hizi ofisi ni muhimu sana."Mkuu wa Wilaya ya kahama Frank Nkinda alipongeza hatua ya vijana hao kukiri makosa yaliyofanywa na baadhi yao wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa oktoba 2025.Nkinda amewaahidi vijana hao pamoja na wananchi wa Kahama kuwa, serikali ipo pamoja nao na kuwataka kuwa wavumilivu wakati serikali inafanya jitihada za kuyarejesha majengo hayo katika hali ya kawaida na kuendelea kuwahudumia wananchi.Amesema "Mmekuwa wazalendo sana, niwapongeze kwa kitendo hiki cha leo, serikali iko pamoja nanyi, tutafanya kazi pamoja ili kurejesha hali ya kawaida katika wilaya yetu. Vijana wenzangu tuache mihemko tunaoumia ni sisi, majengo haya ni ya kwetu sisi wananchi, tumeharibu sasa tunahangaika."Mwisho.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment