" WADAU WA SEKTA YA MILKI MWANZA WAHIMIZWA KUZINGATIA SHERIA NA TAALUMA

WADAU WA SEKTA YA MILKI MWANZA WAHIMIZWA KUZINGATIA SHERIA NA TAALUMA

 

MWANZA

Wadau wa Sekta ya Milki mkoani Mwanza wamesisitizwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya taaluma ya milki ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kutoa huduma bora na zenye kuaminika kwa wananchi.

Msisitizo huo umetolewa leo Machi 17, 2026 mkoani Mwanza na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa huo, Bw. Wilson Luge, wakati akifunga kikao kazi cha wadau wa Sekta ya Milki kilichoandaliwa na Kitengo cha Milki kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Amesema mafunzo na semina zinazotolewa kwa wadau wa Sekta ya Milki yana mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa kitaalamu pamoja na kuimarisha utendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi, hususan katika masuala yanayohusu tathmini ya mali na usimamizi wa milki.

“Tunapenda kuishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Milki kwa kutoa semina na mafunzo kwa wadau wetu wa Sekta ya Milki. Mafunzo haya yatawasaidia kuongeza ujuzi na kuimarisha weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku,” amesema Luge.

Aidha, amewasisitiza wadau hao wa sekta ya milki kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na kujiepusha na vitendo vinavyokiuka sheria ikiwemo kujihusisha na masuala ya utakatishaji fedha, huku akielezea umuhimu wa kufuata taratibu zote za kisheria na kitaaluma katika kutoaji huduma za tathmini ya mali.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Milki (Real Estate) inaendesha mijadala ya pamoja na wadau kwa lengo la kupata maoni kuhusu utambuzi na usajili wa Wadau wa Sekta ya Milki ili kuboresha na kukuza sekta ya milki nchini.

Mijadala hiyo inalenga kutoa elimu, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya milki nchini ambapo tayari kitengo hicho kimefanya vikao vya mijadala katika mkoa wa Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Tanga, Mwanza na Morogoro.

Post a Comment

Previous Post Next Post