" WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA SIKU YA MLAJI DUNIANI 2026

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA SIKU YA MLAJI DUNIANI 2026



Na John Bukuku

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mlaji Duniani mwaka 2026 yatakayofanyika Machi 31, 2026, katika Hoteli ya Johari, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo, “Bidhaa Salama ni Msingi wa Imani ya Mlaji.”

Bi Ngasongwa amesema Siku ya Mlaji Duniani huadhimishwa kila Machi 15 duniani kote kwa lengo la kuhamasisha haki na wajibu wa walaji katika soko na kuimarisha uwajibikaji wa wazalishaji na watoa huduma kwa ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa chimbuko la siku hiyo lilitokana na hotuba ya aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy, aliyotoa Machi 15, 1962 katika Bunge la Marekani (Congress), ambapo alibainisha haki za msingi za walaji, hatua iliyopelekea kutambuliwa kwa haki nane za mlaji kimataifa. Maadhimisho rasmi yalianza mwaka 1993, huku FCC ikianza kuyaadhimisha nchini tangu mwaka 2009.

“Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, tunasisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa sokoni ni salama, zina viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, na zinajenga imani kwa walaji,” amesema Bi Ngasongwa.

Ameongeza kuwa bidhaa bora huchangia ukuaji wa uchumi imara kwa kuwa walaji wanapata thamani ya fedha zao, huku wafanyabiashara wanaozingatia ubora wakinufaika na ushindani wa haki unaochochea ubunifu na ufanisi.

Kwa mujibu wa Bi Ngasongwa, mashirika ya kimataifa yameendelea kusisitiza usalama wa bidhaa hususan katika biashara mtandao kutokana na changamoto za ukosefu wa uwazi na bidhaa kutokidhi viwango vinavyotakiwa. Amebainisha kuwa United Nations Conference on Trade and Development (UNCTAD) Desemba 16, 2025 ilipitisha kanuni mpya za kimataifa za usalama wa bidhaa zijulikanazo kama New Global Consumer Product Safety Principles ili kuimarisha ulinzi wa walaji katika masoko ya kawaida na ya mtandao.

Nchini Tanzania, amesema FCC imefanya utafiti uitwao Consumer Protection Assessment on E-Commerce Business in Mainland Tanzania kwa lengo la kutathmini ulinzi wa walaji katika biashara mtandao na kusaidia maamuzi ya kisera.

Amesema katika kipindi cha maadhimisho hayo, FCC itatoa elimu kwa umma kupitia televisheni na redio za kitaifa na kijamii, kuandaa kliniki za walaji katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Musoma, Njombe na Tanga, pamoja na kuendesha semina kwa wafanyabiashara na taasisi zinazotumia mikataba ya walaji (Standard Form Consumer Contracts).

Bi Ngasongwa amewahimiza wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa na huduma kwa kudai risiti, kusoma maelekezo ya matumizi na kutoa taarifa FCC wanapokutana na bidhaa zisizo salama au zenye upotoshaji.

“Tunawaomba wananchi wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya, kufika katika kliniki za walaji na kutoa changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Ametangaza rasmi kuanza kwa Maadhimisho ya Siku ya Mlaji Duniani 2026 nchini na kuwataka wadau wote kushirikiana katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu kwa vitendo ili kujenga uchumi imara na endelevu kwa ustawi wa Watanzania.

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post