" GERTRUDE MONGELA AZUNGUMZIA NGUVU YA MAJADILIANO KATIKA KUTATUA MIGOGORO

GERTRUDE MONGELA AZUNGUMZIA NGUVU YA MAJADILIANO KATIKA KUTATUA MIGOGORO



Na Beda Msimbe BSKY Media

Mwanasiasa na mwanadiplomasia wa kimataifa, Gertrude Mongela, ambaye amewahi kuhudumu kama Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake, anabainisha kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya lawama kati ya wazee na vijana. 

Katika mahojiano Maalumu na BSKY Media, Mongela anasisitiza kuwa sote kama binadamu tumetikiswa na mabadiliko ya tabia nchi, uchumi, siasa, na teknolojia. Mabadiliko haya yanatupasa kujitathmini upya ili kuendeleza jamii bila kusigana, kwani majadiliano ndiyo msingi mkuu wa kupunguza hali ya sintofahamu na kutengeneza fursa za kujitegemea.

Akilinganisha malezi ya zamani na ya sasa, Mongela anabainisha kuwa uhusiano wa mzazi na mtoto umepungua kutokana na mabadiliko ya kijamii. Anakumbuka jinsi zamani mtoto alivyokuwa akilelewa mgongoni mwa mama yake, akihisi joto na upendo wa moja kwa moja, tofauti na sasa ambapo watoto wengi hulelewa na walezi wengine. 


Hali kadhalika, alizungumzia mfumo wa mamlaka ya baba nyumbani kuwa umeyumba; zamani baba alikuwa na sauti na kauli iliyosimamiwa kwa nidhamu, jambo lililomfanya kijana kuwa na mipaka na matumaini ya wazi kuhusu mustakabali wake. Leo hii, vijana wanahitaji zaidi ya matumaini tu ili kukabiliana na ugumu wa maisha, ikiwemo changamoto za mahusiano na ndoa ambazo zinahitaji jamii kujitafakari upya.

Kuhusu mivutano kati ya vizazi, Mongela anatoa onyo dhidi ya tabia ya wazee kuwalaumu vijana pekee, akisema kuwa kufanya hivyo ni kuwaonea kwani hata baadhi ya wazee "walishavurugwa." 

Anasitiza umuhimu wa kutumia busara badala ya lawama kwa kurejea kisa cha mzee mmoja huko Ukerewe wakati akiwa mbunge ambaye alikiri kuwa, kama changamoto za sasa (wakati huo katika mkutano wa hadhara walikuwa wanazungumzia ukimwi) zingetokea wakati wa ujana wake, naye ugonjwa ungemkumba. 

"Hii inatufundisha kuwa badala ya kunyoosheana vidole, pande zote mbili zinapaswa kukaa pamoja na kutumia fursa za majadiliano zilizopo ili kupata utulivu na kusonga mbele kwa pamoja." alisema.

Akigusia harakati za kudai uhuru na usawa, Mongela anatoa mifano ya wanawake shujaa kama Binti Matola na Amina, ambao walitumia nguvu ya hoja na ujasiri bila fujo kuleta mabadiliko. 

Binti Matola alipinga muda mrefu uliowekwa na wakoloni kwa kutumia mithali nzito, jambo lililochochea vuguvugu la uhuru wa Tanzania kuwahi kufika mwaka 1961 badala ya 1971. 

Mongela anafundisha kuwa ujasiri wa kweli si kufanya fujo au vurugu, bali ni uwezo wa kufikiri na kusema kwa namna inayoleta mabadiliko chanya. Anatoa wito kwa jamii kutumia majukwaa yaliyopo kama makanisa, misikiti, na kamati za bunge kujadili ajenda za kitaifa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post