" MAAFISA ARDHI WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA

MAAFISA ARDHI WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA






Na Mwandishi Wetu

Aprili 14, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang’, shauri la uhujumu uchumi namba 7891/2026 limefunguliwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Arnold Kileo, likiwakabili Maafisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Bw. Erick Erasmus Mbeya na Bw. Egidius Sweetber Kashaga.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka wakiwa watumishi wa umma, kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2023.

Mwendesha mashtaka kutoka TAKUKURU Wilaya ya Hanang’, Bw. Daudi Kingazi, ameieleza mahakama kuwa washtakiwa walitumia vibaya madaraka yao kwa kuhamisha, kusajili na kutoa hati ya kiwanja kwa mtu mwingine, kinyume na kifungu cha 187(1)(d)(i) cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113.

Washtakiwa wote wawili wamesomewa mashtaka yao na kukana kutenda kosa hilo. Hata hivyo, wamefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kwa sasa wapo nje kwa dhamana huku shauri hilo likiahirishwa hadi Mei 5, 2026 kwa ajili ya kusomwa kwa hoja za awali (PH).

Post a Comment

Previous Post Next Post